Kiongozi wa chama cha CDU, Friedrich Merz, kugombea ukansela
18 Septemba 2024Uteuzi huo umetangazwa Jumanne katika mkutano na waandishi wa habari jijini Berlin. Merz alikuwa pamoja na Markus Soeder, kiongozi wa chama kidogo cha CSU ambaye pia alikuwa na nia ya kugombea ukansela. Chama hicho cha CSU kinafungamana na chama cha CDU.
Soma Pia: Kiongozi wa CSU yuko tayari kuwania ukansela
Katika wiki za hivi karibuni, Soeder aliweka wazi nia yake ya kutaka kugombea ukansela, ingawa katika sheria ya jadi ya vyama ndugu vya CDU/CSU, kiongozi wa CDU ndiye hupewa nafasi ya kwanza katika muungano huo ya kuamua iwapo atagombea ukansela.
Soeder, ambaye ni Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria, alitangaza uamuzi huo wa pamoja akisema kwamba swala la nani atakayeviwakilisha vyama va CDU/CSU katika kugombea ukansela limeamuliwa.
Hatua hiyo ya Markus Soedar ya kukaa kando, imefungua njia ya kwenda juu kwa Fredrich Merz, mwenye umri wa miaka 68, anayekiendesha chama chake cha CDU kuelekea mrengo wa kulia tangu alipochukua hatamu za kukiongoza chama hicho mnamo 2022 baada ya kustaafu kansela Angela Merkel aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 16.
Soma Pia: Scholz na upinzani wabumburushana bungeni kuhusu uhamiaji
Kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha CDU mara kwa mara amekuwa akiukashifu muungano wa serikali ya Kansela Olaf Scholz kwa sera yake ya uhamiaji, lakini mara tu alipotangazwa kuwa mgombea wa ukansela wa vyama vya CDU/CSU alisema anatumai kwamba swala hilo halitotawala katika kampeni za uchaguzi mkuu ujao.
Mgombea asiyejulikana bado kwa wapigakura
Merz amesisitiza kwamba wanataka kushinda uchaguzi ujao ili kuwajibika kwa ajili ya nchi ya Ujerumani na kwamba wataweka sera ambazo zitaipelekea mbele Ujerumani na kuwafanya watu wajivunie tena nchi yao.
Uamuzi huo wa vyama vya CDU/CSU wa kumteua Merz kugombea ukansela unaweka mazingira ya kuipa changamoto serikali ya mrengo wa kushoto ya Kansela Olaf Scholz katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Septemba mwaka ujao wa 2025.
Kwa sasa kambi ya wahafidhina inaongoza katika kura za maoni, mbele ya muungano wa vyama vitatu vinanvyoongoza serikali ambavyo ni Social Democrat (SPD) cha Kansela Olaf Scholz, Chama cha Kijani na Chama cha Waliberali, (FDP).
Friedrich Merz anaweza kuwa maarufu katika chama chake cha CDU lakini hajulikani sana miongoni mwa wapiga kura wengi.
Soma Pia: Kansela Scholz atetea mipango ya pensheni katika bajeti ya 2025
Kura ya maoni ya mwishoni mwa wiki iliyofanywa na taasisi inayoshughulikia maswala ya kijamii, INSA, ilionyesha asilimia 25 pekee ya wapiga kura wangemchagua Merz kama kansela na asilimia 21 wangelimchagua Olaf Scholz, endapo uchaguzi ungefanyika wakati huu. Kura hiyo ya maoni imeonesha asilimia 48 ya wapiga kura hawangemchagua yoyote kati ya wagombea hao wawili.
Ndio maana chama cha CDU kimesema uamuzi wa mapema,wa kumchagua mgombea wa ukansela mwaka mmoja kabla ya uchaguzi unalenga kuepusha mzozo na kujirudia makosa kama yaliyofanyika katika kampeni ya uchaguzi ya mwaka 2021 ambapo vyama vya wahafidhina vya CDU/CSU vilipata matokeo mabaya zaidi kuwahi kutokea.