CDU-CSU wazinduwa ilani ya uchaguzi wa Septemba
22 Juni 2021Armin Laschet, kiongozi wa chama cha CDU cha Kansela Angela Merkel na mtu anayeangaliwa kama mrithi wake, alisema mara tu baada ya kuizindua ilani hiyo siku ya Jumatatu (Juni 21) kwamba muungano huo unataka kuwa mshiriki wa kivitendo wa zama zinazobadilika, ingawa akisisitiza usalama wa Wajerumani kuwa jambo la msingi kwenye mabadiliko hayo.
Awali, viongozi wa CDU na mshirika wake mkuu, chama cha CSU cha jimbo la Bavaria, walikuwa wameipitisha ilani hiyo yenye kurasa 139 ikiwa na jina: "Programu ya Utulivu na Usasa. Pamoja kwa Ujerumani ya Kisasa."
Laschet alisema programu hiyo imechanganya masuala ya ulinzi wa tabianchi na nguvu za kiuchumi pamoja na usalama.
Mkuu wa chama cha CSU, Markus Soeder, ameahidi kupitiwa upya kwa bajeti ya Ujerumani baada ya uchaguzi wa Septemba, akisema ni wakati huo ndipo itakuwa wazi sehemu zipi za mpango wao zinaweza kutekelezwa na kwa namna ipi.
Fursa mpya za kukuza uchumi
Wakati huo huo, Laschet aliahidi kupunguza kile kinachoitwa utepe mwekundu, yaani urasimu serikalini, kulegeza vikwazo vya biashara na kuunda fursa mpya kwa ajili ya ukuwaji uchumi, hatua ambazo zitachochea makusanyo makubwa zaidi ya kodi na hivyo kuviwezesha vyama hivyo kutekeleza mipango yao.
Kansela Merkel, ambaye anastaafu rasmi mwezi Septemba baada ya kushikilia wadhifa huo tangu mwaka 2005, ameisifia ilani hiyo akisema Ujerumani ilikabiliwa na mabadiliko makubwa kutokana na janga la corona, na ilikuwa muhimu kwa vyama vyao kuzungumzia mabadiliko hayo kwa nguvu.
Muelekeo kuhusu China
Katika masuala ya kimataifa, ilani hiyo inaitaja China kama mshirika, mshindani na hasimu, sera inayoakisi muelekea wa mataifa ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuelekea taifa hilo kubwa kiuchumi.
Merkel alikuwa akipigia debe mafungamano ya kibiashara na China kwa miaka kadhaa na alikuwa mstari wa mbele kusaka makubaliano ya uwekezaji kati ya Beijing na Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwaka 2020.
Lakini kwa sasa, mtazamo wa Ujerumani unabadilika, huku mkataba wa uwekezaji ukiwa umesahaulika na sasa manifesto ya CDU/CSU unalielezea taifa hilo la Asia kama changamoto kubwa kabisa kwenye sera za nje na usalama.
Endapo muungano wa CDU/CSU utashinda kama inavyotazamiwa, basi manifesto hii ndiyo itakuwa msingi wa mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto na vyama vingine.