Laschet na Soeder wawania nafasi ya Merkel
12 Aprili 2021Armin Laschet wa Christian Democratic Union - CDU na Markus Soeder, mkuu wa chama dada cha Christian Social Union – CSU, wamesema wako tayari kuuongoza muungano huo wa siasa za wastani za mrengo wa kulia katika uchaguzi wa Septemba.
Maafisa wakuu wa CDU wanakutana leo mjini Berlin kujadili hatua zinazofuata wakitafuta kuanza enzi mpya baada ya Merkel katikati mwa uungaji mkono wa umma unaopungua.
Wakati uongozi wa chama hautarajiwi kutoa haraka uamuzi wa mwisho kuhusu mgombea wao wa ukansela, wapi utakapoegemea huenda ikawa ishara muhimu ya ni nani muungano huo utamchagua mwishowe. Mkuu wa chama cha Kansela Merkel – CDU Armin Laschetameelezea matumaini kwamba mkutano muhimu leo wa uongozi wa chama utamchagua kuwa mgombea wao wa wadhifa wa ukansela licha ya upinzani kutoka kwa mwenzake wa Bavaria. "Lengo letu ni kuleta umoja kati ya CDU na CSU katika hali ya sasa ya nchi yetu, ambapo kansela anaondoka madarakani. Ulaya inafuatilia matukio yanavyobadilika Ujerumani. Ulimwengu unataraji kuiona Ujerumani iliyo imara."
Soma zaidi: Kiongozi wa CSU yuko tayari kuwania ukansela
Laschet, mshirika wa muda mrefu wa Merkel mwenye umri wa miaka 60, alichukua uongozi wa CDU Januari, na kawaida angekuwa chaguo la kwanza la kuviongoza vyama hivyo kuelekea uchaguzi wa Septemba 26, wakati Merkel atakapostafu siasa baada ya miaka 16 akiwa kansela.
Lakini uungwaji mkono wa umma kwa vyama hivyo dada unashuka kuhusiana na jinsi vilivyoushughulikia mgogoro wa corona, na baadhi wamemtaka Laschet kumpisha mkakamavu Soeder mwenye umri wa miaka 54.
Baada ya miezi ya uvumi, Soeder alithibitisha jana nia yake ya kuwa mgombea wa ukansela wa vyama hivyo, kwa masharti kuwa ataungwa mkono na chama chenye nguvu cha CDU. "Kilicho muhimu ni kuwa pia tunaheshimiana. Na naweza kusema hili kutoka mwanzo - bila kujali uamuzi utakavyokuwa mwishowe - tutafanya kazi pamoja vizuri sana sana. kwa sababu hatuangalii maslahi yetu, ni maslahi sio tu ya Umoja wetu - bali ya Ujerumani yote."
Soma zaidi: Maoni: CDU yaendeleza mkondo wa Merkel kwa kumchagua Laschet
Soeder aghalabu humpiku Laschet katika tafiti za maoni, huku utafiti wa karibuni uliofanywa na shirika la utangazaji la umma ARD ukionyesha kuwa asilimia 54 ya Wajerumani wanadhani Soeder anaweza kuwa mgombea mzuri wa ukansela, ikilinganishwa na asilimia 19 tu ya wanaomuunga mkono Laschet.
Muda mfupi uliopita, duru za ndani zimesema uongozi wa CDU umeamua kumuunga mkono Laschet, hatua ambayo inalenga kutouyumbisha muungano wao huo wa kihafidhina kwa ujumla.
AFP/DPA