1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa CSU yuko tayari kuwania ukansela

11 Aprili 2021

Kiongozi wa chama cha kihafidhina cha CSU cha nchini Ujerumani Markus Soeder amesema yuko tayari kuwa mgombea wa ukansela wa muungano wa vyama vyama vya kihafidhina katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba.

https://p.dw.com/p/3rqSM
Deutschland Markus Söder Coronavirus Plenarsitzung Bayrischer Landtag
Kiongozi wa CSU Markus SoederPicha: Sven Hoppe/dpa/picture-alliance

Hayo ni kulingana na wajumbe wanaoshiriki mkutano wa chama hicho walipozungumza na shirika la habari la Reuters.

"Iwapo chama cha CDU kitakuwa tayari kuniunga mkono, nami nitakuwa tayari" amekaririwa Soeder akiwaambia wajumbe wa kikao hicho. Hii ni mara ya kwanza kwa mwanasiasa huyo kuashiria nia yake ya kuwa kansela wa Ujerumani.

Shinikizo linaongeza la kufanyika uamuzi wa mapema juu ya ni nani kati ya kiongozi wa chama cha Christian Democrat (CDU) Armin Laschet au Soeder asimame kupeperusha bendera ya muungano huo wa vyama ndugu katika uchaguzi wa Septemba 26 kumrithi kansela Angela Merkel.

Laschet anaburuta mkia kwenye kura za maoni ya umma

Laschet yuko nyuma ya Soeder kwenye kura za maoni ya umma lakini ana uungwaji mkono wa kutosha wa baadhi ya mawaziri wakuu wa majimbo wenye ushawishi mkubwa.

Deutschland Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: Hannibal Hanschke/AP/picture alliance

Kitamaduni viongozi wa vyama vya CDU na CSU huamua nani atawania kiti cha ukansela lakini baadhi ya wabunge wanashinikiza kuwa na usemi safari hii.

Wakati uchaguzi wa mwezi Septemba unakaribia, wahafidhina wanataka ijulikane mapema nani atakuwa mgombea wao ili kumaliza uvumi unaleta mikawanyiko miongoni mwa wafuasi wa wanasiasa vinara.

"Kama nitazingatia hali ilivyo ndani ya CDU basi uamuzi unapaswa kutolewa haraka" amesema Laschet alipozungumza na gazeti la Bild am Sonntag.

Laschet amesema hakuna uamuzi utakaotolewa kwenye mkutano unafanyika Jumapili lakini kuna hisia kwamba angalau taratibu za mchakato au  ratiba ya kufikia uamuzi vitajadiliwa.

Nani kumrithi Merkel mwezi Septemba?

Laschet mwenye umri wa miaka 60 ni mwanasiasa anayegemea sera za wastani na anazingatiwa kama mgombea atakayeendeleza sera za kansela Merkel ingawa ametofautiana naye kuhusu vizuizi vilivyowekwa na serikali yake kukabiliana na janga la virusi vya corona.

Deutschland | Armin Laschet | Ministerpräsident NRW
Armin Laschet, kiongozi wa chama cha CDUPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mwanasiasa huyo amekwishaweka wazi kuwa anataka kuwa mgombea na kwa nafasi yake ya kuwa kiongozi wa chama kikubwa nafasi yake inaweza kuwa kubwa.

Kwa upande wa Soeder, yeye ana umri wa miaka  54 ni mwanasiasa anayefahamika kwa uwezo wake wa kutumia fursa vizuri na amemuunga mkono Merkel katika hatua alizochukua kupambana na corona.

Wahafidhina wengi wana wasiwasi wa kuingia kwenye uchaguzi wa Septemba 26 bila Merkel ambaye amewaongoza kupata ushindi katika chaguzi nne mfululizo.

Lakini amekataa nafasi ya kuwania muhula wa tano na amejitenga na uwezekano wa kumuunga mkono yeyote kati ya Soeder au Laschet.

Kambi ya wahafidhina imeanguka kwenye kura za maoni hadi asilimia 27 hali ikichangiwa na jinsi serikli ya Merkel inavyoshughulikia kadhia ya Covid-19. Kambi hiyo ilipata ushindi wa asilimia 33 katika uchaguzi wa mwaka 2017.

Wasoshalisti wao wamemteua waziri wa fedha Olaf Scholz kuwa mgombea wao wa ukansela huwa wanachama wa chama cha walinzi wa mazingira watamtangaza mgombea wao mnamo Aprili 19.