1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuhudhuria mkutano wa kimataifa juu ya Syria

10 Januari 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, atakwenda nchini Saudi Arabia kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa kuijadili hali ya Syria baada ya kuondolewa Bashar al-Assad.

https://p.dw.com/p/4p23W
Außenministerin Baerbock in der Türkei
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

 

Mkutano huo utawakutanisha pamoja mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi kadhaa za kanda ya Mashariki ya Kati pamoja na wawakilishi kutoka nchi za Magharibi na pia kutoka Umoja wa Mataifa ambao watakutana katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.

Kulingana na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani mkutano huo wa mjini Riyadh unafuata mkutano uliofanyika katikati ya mwezi Desemba mwaka uliopita huko Aqaba, Jordan na amebainisha kuwa Waziri Baerbock amewasilisha mpango wenye vipengele vinane kwa ajili ya Syria, unaohimiza mabadiliko ya amani katika mfumo wa kisiasa utakaotoa haki na uwakilishi kwa makundi yote katika jamii ya Syria pamoja na kuushughulikia uhalifu wa utawala wa Assad.

Syria I Annakena Baerbock | Ahmad Al-Sharaa | Noel Barrot
Kushoto: Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, wakati wa ziara yake nchini Syria. Katikati: Kiongozi mpya wa syria Ahmad al-Sharaa. Kulia: Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Noel BarrotPicha: Dominik Butzmann/AA/photothek/picture alliance

Wakati wa ziara yake nchini Syria mwanzoni mwa Januari,Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock na mwenzake wa Ufaransa Jean-Noël Barrot waliweka wazi masharti ya msaada wa Umoja wa Ulaya kwa nchi ya Syria.

Mengineyo yaliyotokea nchini Syria siku ya Ijumaa ni kwamba wanawake watatu wamekufa kwenye mkanyagano nje ya Msikiti mmoja mjini Damascus, katika kadhia hiyo watoto watano wamejeruhiwa.

Kikosi cha walinzi wa raia kwenye taarifa yake kimesema mkanyagano huo ni kutokana na msongamano mkubwa kwenye hafla iliyoandaliwa na raia kwenye msikiti wa Umayyad.

Soma Pia: Watu zaidi ya 100 wauawa kaskazini mwa Syria

Chanzo kutoka kwenye shirika la Habari la AP kimesema mkanyagano ulitokea wakati wa kugawa chakula baada ya kumalizika sala ya Ijumaa katika msikiti huo ambapo kutokana na umati mkubwa uliokuwepo polisi walilazimika kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya watu.

Siku ya Ijumaa pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani, alizuru Syria na kuelezea nia ya nchi yake ya kuisaidia Syria katika kujikwamua kutoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na katika kuujenga upya Uchumi wa nchi hiyo uliosambaratika.

Italia | Antonio Tajani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio TajaniPicha: Claudia Greco/REUTERS

Tijani alikutana na viongozi wapya na kusisitiza kuwa utulivu wa Syria na wa nchi jirani ya Lebanon ni lengo la kimkakati la bara la Ulaya na kwamba Italia inataka kuongoza katika ujenzi mpya wa Syria na pia kuwa daraja kati ya Syria na Umoja wa Ulaya kuambatana na maslahi ya kibiashara ya Italia katika Bahari ya Mediterania.

Na Shirika la Kuchunguza Haki za Binadamu la Syria limesema wapiganaji wenye mafungamano na watawala wapya wa nchi hiyo walimnyonga Mazen Kneneh, Ijumaa asubuhi, kwa madai kwamba ni mmoja wa wafuasi wakubwa wa utawala wa zamani wa Bashar al- Assad.

Vyanzo: DPA/AFP