Ulaya kuisaidia Syria ya baada ya Assad
3 Januari 2025Mara tu baada ya kulitembelea gereza lenye historia ya ukatili na mateso la Sednaya kaskazini mwa mji mkuu, Damascus, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot, na mwenzake wa Ujerumani, Annalena Baerbock, waliwaambia waandishi wa habari kwamba nchi zao pamoja na Umoja wa Ulaya kwa ujumla wanaunga mkono serikali ya kipindi cha mpito yenye kuyajumuisha makundi yote.
Mawaziri hao walisema wako tayari kujitolea kikamilifu kwenye ujenzi mpya wa Syria baada ya miongo mingi ya machafuko.
Soma zaidi: Wakuu wa Umoja wa Ulaya wajadiliana vita vya Ukraine na suala la Syria
"Wiki chache zilizopita, matumaini mapya yalizaliwa, matumaini ya Syria yenye mamlaka, yenye utulivu na yenye amani. Ni matumaini tete, lakini ni matumaini ya kweli, na kwa sababu hiyo, Ufaransa itasimama bega kwa bega na Wasyria." Alisema Barrot.
Kwa mujibu wa waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, nchi yake iko tayari kusaidia kwenye uchunguzi wa kile kilichokuwa kinajiri kwenye gereza hilo la Sednaya, hasa kwa kuwa tangu mwaka 2011, Paris ilikuwa ikishirikiana na makundi ya kiraia ya Syria kukusanya taarifa za uhalifu uliokuwa unatendwa na utawala wa Bashar al-Assad.
Ujerumani tayari kushirikiana na Syria
Picha za video zimewaonesha Barrot na Baerbock wakiwa kwenye mazungumzo na mtawala mpya wa Syria, Ahmed al-Sharaa, kwenye kasri lake.
Kwa upande wake, Baerbock, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema Ujerumani ilikuwa inataka kuisadia Syria iwe mahala salama kwa watu wote na dola linalofanya kazi likiwa na mamlaka kamili kwa mipaka yake yote.
Soma zaidi: EU kuanzisha mawasiliano na utawala mpya wa Syria
Alisema ziara yake ni ishara ya wazi kwa Damascus juu ya uwezekano wa mahusiano mapya kati ya Syria na Ujerumani na Ulaya nzima kwa ujumla.
Syria yahakikisha serikali jumuishi
Wakati mawaziri hao wa kigeni kutoka nchi mbili kubwa za Umoja wa Ulaya wakiwa Damascus, mwenzao wa Syria, Asaad Hassan Al-Shibani, alikuwa mjini Riyadh kukutana na uongozi wa Saudi Arabia, ambao aliuhakikishia kwamba serikali mpya ya Syria inadhamiria kuunda utawala unaowajumjuisha wote.
Hapo jana, al-Shibani alikutana na Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia, Khalid bin Salman, mjini Riyadh.
Soma zaidi: Syria: Maelfu wakimbilia kuvuka mpaka wa Ugiriki na Uturuki
"Kupitia ziara yetu, tumewasilisha dira yetu ya kitaifa juu ya uundaji wa serikali inayojikita kwenye ushirikiano na ufanisi na inayojumuisha pande zote, na itakayofanya kazi ya kuanzisha programu ya kiuchumi itakayofunguwa milango ya uwekezaji, ubia, na uimarishaji wa hali za watu wetu." Aliandika kupitia mtandao wa X.
Tangu walipompinduwa Bashar al-Assad mnamo tarehe 8 Disemba, watawala wapya wa Syria wamekuwa wakichukuwa hatua za kuwahakikishia majirani zao na mataifa ya Magharibi kwamba hawana nia ya kuyasafirisha mapinduzi yao ya Kiislamu kwenye mataifa mengine.