Faeser: Baadhi ya Wasyria huenda wakalazimika kurejea kwao
5 Januari 2025Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Faeser amesema sehemu ya Wasyria waliokimbilia Ujerumani wanaweza kulazimika kurudi katika nchi yao kwa masharti na vigezo maalum.
Akizungumza na magazeti ya Ujerumani yanayochapishwa na kampuni kubwa ya Funke, waziri huyo ameweka wazi kwamba idara ya uhamiaji ya Ujerumani itakagua na kubatilisha haki ya kupatiwa hifadhi na ulinzi kwa raia wa Syria kwa sababu hali nchini mwao imetulia. Hata hivyo amesisitiza kwamba hatua hiyo itawalenga pekee wale wasio na haki ya kubakia nchini Ujerumani na haitawahusu Wasyria walio na vibali vya kazi au walioko shuleni.
Soma pia: Hali mbaya ya hewa yaathiri shughuli za ndege Ujerumani
Ofisi ya Wizara za Mambo ya Nje na ya Ndani zinafanya kazi pamoja ili kupata picha kamili ya hali ya kisiasa na kiusulama nchini Syria kufuatia kupinduliwa kwa mtawala wa muda mrefu Bashar al-Assad.
Kwa sasa takriban Wasyria 975,000 wanaishi Ujerumani, kulingana na takwimu kutoka wizara ya mambo ya ndani. Wengi waliwasili baada ya mwaka 2015 kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.