1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Wasyria wapate haki baada ya Assad kuanguka

Hawa Bihoga
9 Januari 2025

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Geir Pedersen ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba Wasyria wanahitaji kupata haki kwa awamu nyingine baada ya kuanguka kwa utawala wa zamani mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/4oyUw
Syria | Mjumbe Maalum wa UN | Geir Pedersen
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Geir Pedersen Picha: Andrew Caballero-Reynolds/Pool via REUTERS

Katika mkutano wa baraza hilo uliofanyika hapo jana Jumatano Pedersen alisisitiza kuwa licha ya kuwepo kwa kile alichokiita "fursa kubwa" lakini pia kuna "hatari ya wazi" katika wakati huu ambapo Syria inaingia katika utawala mpya.

Aliongeza kuwa, pamoja na ukweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo sheria na utaratibu unachukua nafasi yake, lakini bado walishuhudia matukio mengi ya uvunjifu wa amani katika mikoa ya pwani na hasa Homs na Haman ikiwemo vitendo vya udhalilishaji uliovuka mipaka ya kiutu.

Soma pia:Assad ameondoka: Je, Syria bado inastahili kuwekewa vikwazo?

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria alionesha wasiwasi wake mkubwa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kuendelea kwa uwepo wa jeshi la Israel ndani ya Syria na kukiuka mkataba wa mwaka 1974 unaozuwia kuingilia maeneo yaliotengwa.

"Taarifa za jeshi la Israel kutumia risasi za moto dhidi ya raia, kuwahamisha na kuharibu miundombinu ya raia pia haya yanatia wasiwasi."

Aliongeza kwamba ukiukaji huo, pamoja na mashambulizi ya anga ya Israel katika maeneo mengine ya Syria yaliyoripotiwa hata wiki iliyopita huko Aleppo yanaweza kuhatarisha matarajio ya mabadiliko ya kisiasa yenye tija.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, Thomas Fletcher alisema kwamba wanahitaji hakikisho la mtiririko mzuri wa misaada ndani ya Syria, hii ikiwa na maana kwamba vikwazo vyoyvyote havipaswi kuzuia mwenendo wa uungwaji mkono wa kibinadamu.

Watu 37 wauwawa kwenye shambulio la anga Syria

Ama tukiangazia hali ndani ya Syria mashambulizi ya anga yaliyofanywa na vikosi vinavyoungwa mkono na Uturiki mapema leo Alhamis yamesababisha vifo vya watu 37 katika eneo la kaskazini mwa Syria la Manbij.

Kwa mujibu wa shirika linalofuatilia vita hivyo la Syrian Observatory for Human Rights lenye makao yake nchini Uingereza, wengi wa waliouwawa ni wapiganaji wanaoungwa mkono na Uturiki, lakini pia wapiganaji sita wa KikurdI pamoja na raia.

Aidha, shirika hilo limeongeza kwamba takriban watu 322 wameuawa kwenye mapigano katika eneo hilo la Manbij tangu mwezi uliopita.

Syria: Wafungwa chini ya utawala wa Assad waachiwa huru

Soma pia:Faeser: Baadhi ya Wasyria huenda wakalazimika kurejea kwao

Mapigano ya hivi karibuni zaidi yameripotiwa licha ya Marekani kusema Jumatano kwamba inajitahidi kushughulikia wasiwasi wa Uturuki nchini Syria ili kumzuia mshirika huyo wa NATO kuzidisha mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi.

Siku ya Jumatano Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken alisema Uturuki ina "wasiwasi halali" kuhusu wanamgambo wa Kikurdi ndani ya Syria na kutoa wito wa azimio nchini humo ambalo ni pamoja na kuondoka kwa "wapiganaji wa kigaidi wa kigeni".

Hapo jana Jumatano akiwa mjini Paris, Waziri Blinken alisema Marekani imeungana na mataifa mengine ya Ulaya katika kuleta amani na utulivu nchini Syria, ikiwa ni mwezi mmoja baada ya kundi la waasi kumuangusha mtawala wa muda mrefu Bashar al-Assad.