Vita kusitishwa kwa muda mashariki mwa Kongo
5 Julai 2024Ikulu ya Marekani ya White House imesema makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yatakayoanza kutekelezwa leo Ijumaa kuanzia saa sita usiku na kuendelea hadi Julai 19, yatayahusisha maeneo ambayo migogoro huwaathiri zaidi raia.
Marekani yasema mashirika ya msaada yanashindwa kufikia eneo la mgogoro
Katika taarifa, msemaji wa baraza la usalama la kitaifa la Marekani Adrienne Watson, amesema kuongezeka kwa mapigano katika siku za hivi karibuni zaidi katika jimbo laKivu Kaskazini kumewazuia wafanyakazi wa mashirika ya msaada kufikia maelfu ya wakimbizi wa ndani katika eneo karibu na Kanyabayonga na kusababisha zaidi ya watu 100,000 kuyakimbia makazi yao.
Kongo na Rwanda zaunga mkono usitishaji vita mashariki mwa Kongo
Watson ameongeza kuwa serikali za Kongo na Rwanda zilielezea kuunga mkono makubaliano hayo ili kupunguza mateso kwa watu walio katika mazingira magumu na pia kuweka masharti kwa ajili ya kupunguza kwa kiasi kikubwa mvutano mashariki mwa Kongo.
Taarifa hiyo imesema Marekani inatoa wito kwa pande zote kuheshimu makubaliano hayo.
Eneo la Kivu Kaskazini limekuwa likipambana na uasi wa kundi la M23 kwa zaidi ya miaka miwili pamoja na vurugu nyingine za makundi ya wapiganaji.
Mara kwa mara, Kongo,Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi yameishutumu Rwanda kwa kuliunga mkono kundi hilo la M23 kwa msaada wa wanajeshi wake pamoja na silaha, madai yanayokanushwa na nchi hiyo.
Ulanguzi wa binadamu mashariki mwa Kongo waibua hofu
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa walioidhinishwa na Baraza la Haki la Umoja wa Mataifa, wameelezea kushangazwa na idadi iliyoripotiwa ya takriban wahanga 531 wa unyanyasaji wa kijinsia unaohusishwa na migogoro kutoka Agosti 2023 hadi Juni 2024, katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri, Tanganyika na Maniema.
Soma pia: Wanamgambo waua takriban watu 23 mashariki mwa DRC
Wataalamu hao wamesema tuhuma zilizowasilishwa kwao, zinaelezea kuhusu wanawake na wasichana waliotekwa nyara kwa madhumuni ya ukatili wa kijinsia au unyanyasaji wa kingono, wakati wakitafuta chakula au kuni au kushiriki katika shughuli za kilimo.
Wataalamu hao wameongeza kuwa ripoti za kuhusika kwa vikosi vya ulinzi na usalama zinaibua wasiwasi mkubwa.
Wataalamu wa UN waelezea hofu ya kuondoka kwa MONUSCO Kongo
Wataalamu hao pia wameelezea wasiwasi kuhusu kukatizwa kwa operesheni ya Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO.
Wameelezea wasiwasi wao kwamba kwa kuondoka kwa kikosi hicho, masuala muhimu ya mifumo ya tahadhari ya mapema ya ukiukaji wa haki za binadamu hayatakuwepo.
Soma pia:Kikosi cha MONUSCO chaondoka rasmi Kivu Kusini
Hivi karibuni, ujumbe wa MONUSCO ulijiondoa kutoka jimbo la Kivu Kusini na unatazamiwa kuondoka Kivu Kaskazini na Ituri, majimbo mawili ya mwisho ambapo bado ujumbe huo unatekeleza majukumu yake ijapokuwa tarehe bado haijatajwa.