1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Waasi wa M23 waendelea kukamata miji muhimu ya Kongo

4 Julai 2024

Waasi wa M23 wameikamata miji ya Kanyabayonga na Kirumba mashariki ya Kongo. Ukosefu wa shinikizo la kimataifa na hali ngumu ya jeshi la Kongo vilisaidia mafanikio yao, watalaamu wameiambia DW.

https://p.dw.com/p/4hrkc
Waasi wa M23
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likipigana na waasi wa M23 mashariki mwa nchiPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mzozo unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na katika kanda nzima ya Maziwa Makuu umeongezeka na kusababisha maelfu ya watu kukimbia maskani zao na kuibua wasiwasi mkubwa juu ya hali ya kiutu hasa katika Mkoa wa Kivu Kaskazini, ambako kundi la waasi wa M23 limeendelea kuteka maeneo

Mnamo Juni 28 na 29, waasi wa M23 waliiteka miji ya Mashariki mwa Kongo ya Kanyabayonga na Kirumba, mtawalia. Wakaazi wa Kirumba kama Tsongo Augustin wanasema watu zaidi na zaidi wamelaazimika kuondoka eneo hilo ambalo lilikuwa limegeuka nyumbani kwa watu wengi waliohamishwa tayari na mzozo huo. Augustin alisema Kirumba ilizikaribisha familia nyingi zilizokosa makaazi kutoka wilaya ya Rutshuru na hivi sasa wanalaazimika kukimbia tena. Kirumba ndiyo eneo kubwa zaidi la makaazi katika wilaya ya Lubero, ikiwa na wakaazi zaidi ya 120,000.

Mzozo wa wakimbizi Kongo
Watu wakusanyika katika eneo la mlipuko katika kambi ya wkaimbizi viungani mwa Goma, Kongo Mei 2024Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Kanyabayonga kwa upande mwingine ni nyumbani kwa zaidi ya watu 60,000, lakini mamia ya maelfu ya watu walikuwa wamekimbia katika miezi ya karibuni, kutokana na kusonga mbele kwa waasi. Profesa Adolphe Agenonga Chober, mhadhiri wa chuo kikuu cha Kisangani, ambaye pia ni mataalamu wa mavuguvugu ya makundi yanayobeba silaha, anasema jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Afrika zimesalia kimya kuhusu mzozo huu kutokana na maslahi yanayotofautiana. Jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Afrika zinahimiza majadiliano kati ya pande zinazoshiriki mzozo huu, mkakati ambao unapingwa na serikali mjini Kinshasa.

Eneo la kimkakati

Tshisekedi: Amani imo mikononi mwa rais atakayemrithi Kagame

Kwa mujibu wa Profesa Agenonga, eneo hilo linazingatiwa kama ngome ya kimkakati, ambayo inakusudiwa kuwazuwia waasi kusonga mbele kuelekea kanda kuu ya kaskazini mwa nchi hiyo. Kutekwa kwa Kanyabayonga na Kirumba sasa kumesababisha uhamaji mwingine wa watu wengi na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu.

Wengine wanahisi kuvunjwa moyo na walioko madarakani. Wema Kennedy, mkaazi wa Kirumba alilalamika kwamba jamii yake haioni serikali ikifanya chochote kuchukuwa udhibiti wa maeneo yaliotekwa na M23. Bunagana kwa mfano imekuwa chini ya M23 kwa karibu miaka miwili sasa, na wengi wanahofia kwamba haitakuwa rahisi kwa serikali kurejesha udhibiti wa Kirumba. Tunahisi kwamba M23 iliyoanza kama kundi dogo, hivi sasa inazidi kila kitu nguvu na kwa sababu hii watu wamevunjwa moyo.

Shambulio la karibuni dhidi ya msafara wa kijeshi mkoani Kivu Kaskazini limechochea zaidi hali ya usalama na mzozo wa kiutu katika eneo hilo na mbali. Wanajeshi wawili wa Afrika Kusini waliuawa katika mashambulizi ya karibuni ya aina hiyo, na wafanyakazi wawili wa misaada pia walithibitishwa kuuawa baada ya kuvamiwa na vijana huko Luboro, waliowashuku kuwa maadui.

Kimya kutoka jumuiya ya kimataifa

Maelfu ya watoto hawaendi shule Kivu Kaskazini

Baraza la Wakimbizi la Norway limekariri juu ukubwa wa mzozo wa kiutu nchini DRC, ambapo mkurugenzi mkaazi wa shirika hilo nchini DRC, Eric Batonon, alisema kunahitajika hatua za haraka kutuliza hali. Ni muhimu sana kwamba jumuiya ya kimataifa na viongozi wote wa dunia wanakuja pamoja kujaribu kutafuta suluhisho kwa mizozo hii, na kuwaruhusu mamilioni ya wanawake na watoto kurejea nyumbani, na kuwalindia mustakabali wao.

Utendaji wa jeshi la Kongo wakati huo umewekwa kwenye darubini, kukiwa na tuhuma za kushindwa kuchukuwa hatua katika mwa mashambulizi yanayoongezeka na mifumo ya uongozi isiyo na ufanisi. Profesa wa sayansi ya siasa kutoka Kongo Mashariki Augustin Muhesi, ametilia mkazo haja ya kutathmini upya mkakati wa jeshi la Kongo.

Katika kuitikia kusonga mbele kwa M23,Rais wa DRC Felix Tshisekedi aliitisha mkutano wa Baraza la Ulinzi na kulihakikishia taifa juu ya dhamira yake ya kulinda mamlaka ya mipaka ya taifa hilo. Hata hivyo ahadi yake inaonekana kuwa tupu wakati ambapo mkoa wa Kivu Kaskazini umekumbwa na vurugu tangu 2021, wakati kundi la M23 lilipoanzisha tena kampeni yake ya mashambulzi mkoani humo.

Waandishi: Wendy Bashi na Mimi Mefo