Hofu DRC juu ya M23 kuiteka miji zaidi wilaya ya Lubero
3 Julai 2024Mapambano ambayo yanaendelea yanaripotiwa kuyakaribia maeneo yaliyo karibu na mji mdogo wa Lubero.
Mapigano hayo ambayo yanaunyemelea mji mkuu wa wilaya ya Lubero, yalianza wiki iliyopita, baada ya waasi wa M23 kuteka miji midogo na muhimu ya Kanyabayonga, Kirumba na Kaseghe.
Duru kutoka uwanja wa mapambano zimedokeza kuwa raia wengi wamekimbia makaazi yao na kuelekea Lubero pamoja na viunga vyake.
Na taarifa ambazo hazijathibitishwa bado zadokeza, kwamba kwa sasa wapiganaji wa M23 wanajaribu kukteka kijiji cha Kitsombiro, ambacho sio mbali sana na mji mdogo wa Lubero ambao pia ni makao makuu ya mkuu wa wilaya hiyo.
Soma pia: Msafara wa misaada ya kibinadamu washambuliwa mashariki mwa Kongo
Mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji mdogo wa Lubero Muhindo Tafuteni, hapa anatuambia kunakoendelea mapigano.
"Kuna mapigano katikati ya vijiji vya Matembe na Vutsorovya. Yaani wamekuwa wakipigania Kaseghe na Matembe kwa siku mbili sasa. Wakimbizi kila mtu anatoroka kwa upande wake na hakuna kambi walimopokelewa. Wakimbizi wanaopokelewa vizuri ni wale waliowasili Kitsombiro. Ni wale hasa walio na namna yakukimbilia huko. Tunaomba serikali kuona jinsi yakutuokoa na hasa kwakushambulia adui kwani jeshi la serikali likiwa halishambilii adui, adui huyo anasonga mbele."
Mapigano baina ya majeshi ya Congo na wapiganaji wa M23 yakiwa yameshasababisha watu wengi kutoroka vijiji vyao, wakimbizi hao wanaishi bila ya msaada wowote ule kama anavyotoka kusema mwenyekiti wa mashirika ya kiraia Lubero.
Na ilikuyapelekea mashirika ya kiutu kuwasaidia wakimbizi katika mji mdogo wa Lubero pamoja na viunga vyake, mkuu wa wilaya hiyo canali Kiwewa Mitela Alain, ametoa mwito kwa vijana kutokabiliana na wafanyakazi wa mashirika ya kiutu ambayo yamekuwa ya kiwasaidia kwa muda mrefu sasa, pale akiwaambia kwamba mashirika hayo sio maadui wa nchi.
"Hamna msaada wowote ule kwa wakombizi. Tunayo shida kubwa na mashirika ya kiutu. Kuna makundi ya vijana ambao wamekuwa wakali dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya kiutu. Hali imekuwa mbaya na inakatisha tamaa. Nikachokiomba raia nikuwa na imani na serikali, kuwa na imani na jeshi na kuwa pia na imani na watu wa mashirika ya kiutu. Ni kwa muda mrefu ndio mashirika hayo yanatusaidia na lah hasha hawawezikuchukuliwa kama adui."
Nayo hali ikiwa ya wasiwasi katika vijiji ambako wanakimbilia wakaazi wanaohofia maisha yao, ripoti toka Ndoluma zasema, kwamba askari wanaotoroka vita walijihusisha na vitendo bya uporaji wa mali za raia.
Na ilikuwaadhibu askari wanaotoroka, mahakama ya kijeshi inaandaa kuwafungulia kesi katika mji wa Lubero ili watakaokutwa na hatia wahukumiwe.
Kusonga mbele kwa kasi kwa waasi wa M23, kumewakatisha tamaa wakaazi wa miji ya Beni na Butembo.
Na ili kuwatia kishindo viongozi wa serikali mjini Kinshasa, wabunge wa Kivu ya Kaskazini, wamekuwa wakikutana kwa mazungumzo na mawaziri wa ulinzi pamoja na yule wa mambo ya ndani kuwapatia ripoti kamili ya hali ya mapigano.