SIPRI: Mapato ya makampuni makubwa ya silaha yapungua
4 Desemba 2023Mapato ya makampuni makubwa ya uzalishaji wa silaha ulimwenguni yalishuka mwaka 2022, licha ya vita vya Urusi nchini Ukraine sambamba na juhudi za mataifa mengi ya ya Ulaya za kuongeza matumizi ya ulinzi.
Kulingana na ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa masuala ya Amani iliyoko Stockholm, SIPRI mapato ya makampuni 100 yalishuka kwa ailimia 3.5 ikilinganishwa na mwaka 2021, yalipofikia dola bilioni 597.
Licha ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine pamoja na mivutano katika maeneo mbalimbali ulimwenguni, kuchochea mahitaji makubwa kabisa ya silaha kwa mwaka 2021, ripoti ya SIPRI imeonyesha kuwa makampuni hayo makubwa yalishindwa kuzalisha kiwango kikubwa cha silaha kulingana na mahitaji hayo. Lakini pamoja na hayo, mapato ya makampuni hayo 100 makubwa zaidi ya ulinzi ulimwenguni yaliongezeka ikilinganishwa na mwaka 2015.
Soma pia:Ripoti: Ukraine yawa muagizaji wa tatu wa silaha duniani, 2022
Mkurugenzi wa utafiti wa silaha kwenye Taasisi hiyo Lucie Béraud-Sudreau amesema makampuni mengi yalikabiliwa na vizingiti katika kuongeza uzalishaji, ingawa yalipokea maombi ya kuzalisha silaha zaidi na hasa risasi, na pengine hatua hii itayafanya kupata faida kubwa zaidi katika siku za usoni.
Makampuni ya Urusi na Marekani ndiyo yalikabiliwa na anguko kubwa zaidi kimapato. Kulingana na SIPRI, makampuni ya Marekani yalipata kiwango jumla cha mapato kilichofikia dola bilioni 302, ambacho kimeshuka kwa asilimia 7.9 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Makampuni hayo ya Marekani aidha yalikumbwa na changamoto za usambazaji, yaliyochangia zaidi ya nusu ya mapato yote katika ripoti hiyo ya SIPRI.
Makampuni ya Mashariki ya Kati na Asia ya Mashariki yalijiandaa kukidhi ongezeko la mahitaji
Hata hivyo, kulingana na Taasisi hiyo, takwimu za makampuni ya Urusi haziko wazi sana, na ni makampuni mawili tu ya nchini humo yalihusishwa kwenye ripoti yake hii ya mwaka 2022. Mapato ya makampuni hayo yalishuka kwa asilimia 12.
Lakini nchini Ujerumani, mapato ya makampuni manne yaliyomo kwenye orodha ya SIPRI, yameonyesha wastani wa ongezeko jumla la asilimia 1.1. Makampuni mengine yaliyoshuhudia ongezeko la mapato ni ya nchini Israel, Uturuki na Korea Kusini na China, ambayo makampuni yake yalijikusanyia mapato kwa asilimia 18. Mtafiti wa SIPRI, Xiao Liang amesema makampuni ya China, India, Japan pamoja na Taiwan yamenufaika kutokana na uwekezaji endelevu wa serikali zao zilizoongeza maboresho kwenye majeshi yao.
Soma pia:SIPRI: Idadi ya silaha za nyuklia kuongezeka duniani
Aidha imesema, makampuni ya Mashariki ya Kati na Asia ya Mashariki pia yalikuwa yamejiandaa vyema kukidhi ongezeko la mahitaji ya silaha.
Hata hivyo, makampuni ya uzalishaji wa silaha kwa ujumla yalikabiliwa na upungufu wa rasilimali, athari za mfumuko wa bei na ongezeko la gharama, upungufu wa wafanyakazi na athari zilizoletwa na janga la UVIKO-19 kwenye usambazaji.
Soma pia:SIPRI: Mauzo ya silaha ulimwenguni yamepungua kidogo