Ripoti ya SIPRI: Matumizi ya kijeshi yaongezeka duniani kote
24 Aprili 2023Ripoti ya kila mwaka ya taasisi ya kimataifa ya utafiti wa masuala ya amani ya mjini Stockholm, SIPRI, inasema bajeti za kijeshi ziliongozeka kwa asilimia 3.7 mnamo mwaka 2022 kulinganisha na manunuzi ya mwaka uliotangulia. Mtaalamu aliyeshiriki katika kuandika ripoti hiyo Nan Tian ameiambia DW kwamba nchi ziliongeza manunuzi ya silaha bila ya kujali hali ya kiuchumi ni mbaya au nzuri. Baada ya Urusi kuivamia Ukraine nchi nyingi za Ulaya zimekuwa zinaongeza bajeti zao za kijeshi.
Katika nchi za mfungamano wa kijeshi wa NATO, bajeti za kijeshi zilianza kuongezeka mnamo mwaka 2014 baada ya Urusi kukiteka kisiwa cha Ukraine cha Crimea sambamba na kuwaunga mkono waliojitenga mashariki mwa Ukraine. Nchi wanachama wa NATO zimeamua kuongeza matumizi ya kijeshi kwa asilimia 2 hadi mwaka ujao.
Tazama:
Licha ya manunuzi ya silaha kufikia Euro trilioni 2 duniani kote kiasi hicho kinawakilisha asilimia 0.1 ya pato jumla. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita India, China na Israel zimekuwa zinaongeza bajeti zao za kijeshi. Katika kipindi hicho China iliongeza bajeti ya ulinzi kwa asilimia 63, India kwa asilimia 47 na Israel kwa asilimia 26. Hata hivyo mfumuko wa bei umesababisha kupungua kwa bajeti za kijeshi kulinganisha na uwiano wa tija ya kiuchumi. Uwezo wa kununua umepungua kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa za mahitaji ya kila siku.
Soma:Ripoti: Ukraine yawa muagizaji wa tatu wa silaha duniani, 2022
Kuongezeka kwa bei ya maziwa maana yake pia ni kuongezeka kwa bei ya ndege za kivita. Ripoti ya taasisi ya utafiti wa masuala ya amani ,SIPRI inabainisha hali hiyo. Kupanda kwa gharama za maisha pia ni tatizo kubwa nchini Ujerumani. Kutokana na vita vya nchini Ukraine jeshi la Ujerumani limetengewa Euro bilioni 100 zaidi katika bajeti yake.
Matumizi ya kijeshi, si kununua silaha tu.Kuongezeka kwa matumizi kunajumuisha pia kutoa msaada wa kijeshi kwa nchi nyingine ambao umefikia kiwango kikubwa kutokana na vita vya nchini Ukraine. Kulingana na utafiti Marekani pekee imeshatoa msaada wa dola bilioni 47 kwa Ukraine.
Soma:Ripoti ya SIPRI: vita vya nchini Ukraine vyasababisha ongezeko katika mahitaji ya silaha
Mnamo mwaka uliopita Marekani ilitumia dola bilioni 877 kwa ajili ya ulinzi. Kiasi hicho kinawakilisha asilimia 39 ya bajeti ya kijeshi ya dunia nzima. China inashika nafasi ya pili kwa matumizi ya dola bilioni 292. Wataalamu wa masuala ya kijeshi pamoja na wanasiasa wa Marekani wanatahadharisha kwamba China inaziba pengo la kijeshi kati yake na Marekani. Hata hivyo nchi hizo zinalenga shabaha tofauti za kijeshi.