SIPRI:Vita vya Ukraine si habari njema kwa kampuni za silaha
5 Desemba 2022Kulingana na ripoti mpya kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), watengenezaji wakuu wa silaha duniani wapatao 100 waliongeza mauzo mnamo mwaka 2021, ingawa masuala ya ugavi yameathiri ukuaji wa sekta hiyo. Ripoti iliyochapishwa hii leo (05.12.2022) imebaini kuwa uhaba wa ugavi wa silaha uliosababishwa na janga la COVID-19 umehusishwa na kupungua kwa ukuaji wa sekta hiyo hadi asilimia 1.9 mnamo mwaka 2021 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia 2020.
Taasisi ya SIPRI imetabiri kuwa vita vya Ukraine vinaweza kusababisha matatizo kama hayo katika sekta hiyo hivi karibuni au baadae kidogo. Kutokana na uvamizi wa Urusi na mwitikio wa Ukraine pamoja na washirika wake wa nchi za Magharibi umechochea kuongezeka mahitaji ya silaha, ambapo watengenezaji wamekuwa wakikabiliwa na changamoto katika kutafuta malighafi na vifaa.
Soma Zaidi:SIPRI: Mauzo ya silaha ulimwenguni yamepungua kidogo
Taasisi hiyo ya kimataifa SIPRI, inayojikita kwenye utafiti wa migogoro, silaha, udhibiti wa silaha na upokonyaji silaha, ilibainisha kuwa Urusi ni msambazaji mkuu wa malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa silaha. Hali ambayo inaweza kuwa ndio chanzo cha kukwamisha juhudi za Marekani na washirika wake wa Ulaya katika kuimarisha vikosi vyao vya kijeshi nkutokana na kushindwa kujaza tena hifadhi zao baada ya kupeleka silaha na vifaa vingine vya vita vilivyogharimu mabilioni ya dola nchini Ukraine.
Ripoti hiyo ya SIPRI pia imesema ingawa kampuni za Urusi zimeongeza uzalishaji wa silaha kwa sababu ya vita hata hivyo zinakabiliwa na ugumu wa kupata sehemu muhimu za vifaa vya kielektroniki vya kuendeleza vifaa vya mawasiliano, kompyuta, vifaa kwa ajili ya kupatikana huduma za afya, mifumo ya kijeshi, usafiri, nishati safi, na matumizi mengine mengi. Makampuni hayo pia yanaathiriwa na vikwazo vinavyohusiana na vita, kwa mfano linapokuja suala la kupokea malipo.
Soma Zaidi:SIPRI: Idadi ya silaha za nyuklia kuongezeka duniani
Diego Lopes da Silva, mtafiti mkuu wa taasisi ya SIPRI amesema kuongeza uzalishaji huchukua muda na kama usumbufu katika ugavi utaendelea kuwepo unaosababishwa na vita vya Ukraine basi itachukua miaka kadhaa kwa baadhi ya wazalishaji wakuu wa silaha kukidhi mahitaji mapya ya silaha.
Kampuni nyingi za Ulaya ambazo zinahusika na utalaamu wa kijeshi wa maswala ya anga zimeripoti kupata hasara katika mwaka 2021, hasara ambayo imetokana na usumbufu katika usambazaji amesema mtafiti mwingine wa Taasisi ya SIPRI, Lorenzo Scarazzato. Amesema kwa mauzo ya silaha ya dola bilioni 4.5, kampuni ya Rheinmetall iliyo katika nafasi ya 31 ya wauzaji wakuu wa silaha duniani ndio kampuni kubwa zaidi ya silaha nchini Ujerumani lakini, mauzo yake ya silaha yalipungua kwa asilimia 1.7 mnamo mwaka 2021 kwa sababu ya usumbufu uliojitokeza kwenye swala zima la usambazaji.
Soma Zaidi:Ripoti ya SIPRI- matumizi ya kijeshi yaongezeka duniani
Mkurugenzi wa SIPRI anayesimamia matumizi ya kijeshi na mpango wa uzalishaji wa silaha, Lucie Beraud Sudreau, amesema kampuni zote kubwa na ndogo za silaha zimeripoti kuathirika kwa mauzo yao katika mwaka 2021.
Chanzo: DW Page