Jeshi la Nigeria lawaua watu 85 katika shambulizi la droni
5 Desemba 2023Shirika la Kitaifa la kusimamia matukio ya Dharura (NEMA) lilisema katika taarifa kuwa jeshi halikutoa takwimu zozote za majeruhi, lakini wakaazi wa eneo hilo walisema watu 85, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, walifariki.
Ofisi ya Kanda ya Kaskazini Magharibi imepokea maelezo kutoka kwa mamlaka ya eneo hilo kwamba maiti 85 zimezikwa hadi sasa huku jitihada za kutafuta kama kuna miili mingine zikiwa zinaendelea. NEMA pia imesema watu wapatao 66 walikuwa wakipatamatibabu hospitalini, lakini maafisa wa dharura bado wanajadiliana na viongozi wa jamii waweze kutuliza jazba zilizopo waweze kufika kijijini.
Soma zaidi: Boko Haram yaua watu 37 katika shambulio la kigaidi Nigeria
Vikosi vya jeshi la Nigeria mara nyingi hutegemea mashambulizi ya anga katika mapambano yao dhidi ya wanamgambo wa Kaskazini Magharibi na Kaskazini Mashariki mwa nchi, ambapo wanajihadi wamekuwa wakiendesha uasi kwa zaidi ya muongo mmoja.
Ofisi ya rais katika taarifa yake ilisema,Rais Tinubu amepokea tukio hilo kwa masikitiko na maumivu, na amehuzunishwa na Wanigeria wengi kupoteza maisha. Jeshi kwa upande wake liliripoti kuwa ndege yake isiyo na rubani ilikuwa misheni ya kawaida ambapo iliathiri watu wa jamii bila kukusudia.
Kwa mujibu wa mkazi wa eneo hilo Idris Dahiru ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) ''Alikuwa ndani ya nyumba wakati bomu la kwanza liliporushwa, na wakatoka kukimbilia eneo la tukio ili kusaidia walioathirika na ndipo liliporushwa bomu la pili''. Shuhuda huyo pia amesema, katika tukio hilo shangazi yake, wake wanne wa kaka zake na watoto zao sita, walikuwa ni miongoni mwa waliofariki. Na alienusurika alikua ni mtoto mchanga wa kaka yake mkubwa.
Magenge ya wanamgambo kwa muda mrefu yamekuwa yakieneza hofu katika maeneo ya Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria, na kuendesha shughuli zake za kuvamia vijiji na kupora mali kutoka kwenye maficho yao ya misituni.
Wapiganaji wa jihadi wamerudishwa nyuma kutoka eneo walilokuwa wanalishikilia, upande wa Kaskazini Mashariki, licha ya kuwa bado wanaendeleza mapambano kwenye maeneo ya vijijini, kwenye mzozo huo uliodumu tangu mwaka 2009 na kusababisha zaidi ya watu 40,000 kuuawa na milioni mbili kuyakimbia makazi yao.
Muendelezo wa jeshi la Nigeria kuwashambulia raia
Mashambulizi mengine ya kijeshi nchini Nigeria yaliwahi kuwakumba raia kimakosa katika siku za nyuma, ikiwemo shambulio la Septemba 2021 huko Kwatar Daban Masara kwenye ZiwaChadKaskazini Mashariki ambapo, takribani wavuvi 20 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati wanajeshi walipowadhania wavuvi hao kuwa wanamgambo.
Tukio lingine la vifo vya raia lililosababishwa na jeshi Nigerialilitokea Januari 2017, ambapo watu 112 waliuawa wakati ndege ya kivita ilipoipiga kambi iliyokuwa na watu 40,000 waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia za wanajihadi katika mji wa Rann karibu na mpaka na Cameroon, ambapo miezi sita baadae jeshi katika ripoti yake lililaumu kukosekana kwa alama zinazofaa kuwa ndio sababu iliyipelekea shambulizi hilo.