Tanzania yazindua kampeni ya elimu ya kisheria kwa umma
16 Februari 2023Waziri wa katiba na sheria nchini humo, Damasi Ndumaro amesema kampeni hiyo inatekelezwa kwa mara ya kwanza nchini humo na inafanyika sehemu zote mbili za muungano yaani Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.
Huduma hiyo ya msaada wa kisheria ambayo inatolewa bure kwa wananchi inasambazwa kuanzia maeneo ya mjini hadi vijijini ambako ndiko kwenye kiini cha mizozo ya ukosefu wa haki kutokana na wengi wao kuwa na uelewa mdogo wa masuala ya kisheria.
Kampeni hiyo mejikita katika kuwapa uelewa wananchi kuzitambua sheria na haki zao na kisha kuwafungulia mlango juu ya namna ya kuzitekeleza na kupigania haki hizo.
Soma pia:Tume ya Afrika ya haki za binadamu ziarani Tanzania
Maeneo yanayopewa kipaumbele katika awamu hii ya kwanza ya miaka mitatu ni pamoja na masuala yahusuyo unyanyasaji wa kijinsia, haki ya kumiliki ardhi, utatuzi wa migogoro wa njia mbadala na masuala ya haki za binadamu.
Kuminywa haki ndio mzizi wa kampeni
Waziri wa Katiba na Sheria, Damasi Ndumbaro ambaye amezungumza na DW anasema kilio cha wananchi kubinywa haki zaoni cha muda mrefu, lakini sasa mwanga wa matumaini utaanza kujitokeza kupitia mpango huu mpya.
Waziri huyo mwenye dhamana ya sheria na katiba amesema mpango huo umewalazimu pande mbili kuja pamoja kwa maana ya asasi za kiraia zinazotetea haki na serikali, ili kufikia kundi kubwa zaidi.
"Ni kwa mara ya kwanza serikali inaungana na asasi kufanya zoezi kama hili." Aliiambia DW waziri Ndumbaro.
Ameongeza kwamba tayari wamekwishatoa mafunzo kwa watoa msaada wa kisheria katika ngazi ya kijamii wapatao 4,900 na zaidi ya 1,000 kati ya hao wamekwishapata vyeti vyao.
Soma pia:Asasi za kiraia kutoridhishwa na tathmini kuhusu Loliondo
Aidha amesisitiza kuwa mradi huo wa kutoa elimu ya sheria kwa wananchi utaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu nchi nzima, unatarajiwa kuleta tija kwenye jamii hasa katika maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudiwa uelewa mdogo wa masuala ya sheria kwa wananchi.
Asasi za kiraia zaunga mkono juhudi
Hatua hiyo imeungwa mkono na makundi mengi yanayopigania ustawi wa wananchi ikiwamo washiriki wa maaendeleo ambao wameonyoosha mkono kuikaribisha.
Wengi wanaamini kwamba kupitia kampeni hiyo ambayo pia itafanywa kwa njia ya mtandao sasa wananchi watapatiwa nyenzo zitakazowawezesha kuzifikia haki zao.
Kituo cha sheria na haki za binadamu kupitia mkuruguenzi wake mkuu, Anna Henga amesema hatua hiyo inaleta tumaini jingine katika kuwafikia wananchi kwenye mukhtadha wa haki na sheria.
"Hii itakuwa nyongeza kwenye kazi zetu, na tunaahidi kushirikiana na wozara" Alisema Henga alipozungumza na DW.
Soma pia:Mahakama ya EAC yajiandaa kwa rufaa ya Loliondo
Mizozo ya ardhi ambayo wakati mmoja uhusisha kati ya wananchi na taasisi za kiserikali ni mtihani ambao wengi wanasubiri kuona namna kampeni hii itakavyoshughulikia na kupata ufumbuzi wake wa kudumu.