Tume ya Afrika ya haki za binadamu ziarani Tanzania
24 Januari 2023Lengo kuu la ujio wa tume hiyo ni kukusanya taarifa pamoja na kufanya tathimini kuhusiana na haki za watu au jamii za watu wa asili, hasa kwa kuangazia eneo la Loliondo na eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambalo limekuwa mgogoro wa muda mrefu na serikali.
SOMA PIA: Hatua ya Tanzania kuwaondoa Wamasai yazidi kuibua hisia
Eneo la Loliondo na eneo la hifadhi ya Ngorongoro, maeneo yote yakiwa mkoa wa Arusha kaskazini mwa Tanzania, kwa kipindi kirefu yamekuwa yakikumbwa na migogoro inayohusishwa na ardhi, serikali ikitaka kuyahifadhi maeneo hayo kwa ajili ya shughuli za utalii huku wengi wa wakazi asili wa maeneo hayo ambao ni wa jamii ya wafugaji ya maasai, wakilalamika kunyanyaswa kwa kuondolewa katika maeneo yao kwa nguvu, kupigwa, kukamatwa na kuuwawa kwa mifugo.
Kulingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mtandao wa haki za binadamu Tanzania THRDC , tume ya Afrika ya haki za binadamu na watu itayatembelea maeneo hayo kwa lengo la kukusanya taarifa na kufanya tathimini kuhusu haki za binadamu.
SOMA PIA: Kupotea kwa Serengeti - Ardhi ya Wamaasai
Wakili Alais Melau ni mwanaharakati wa haki za binadamu kupitia shirika la kiraia anasema amefurahishwa na ujio wa tume lakini anawasiwasi wa kupatikana kwa taarifa sahihi.
"Kimsingi ni kwamba tumepokea tume, baada ya kuhangaika sana ndio tuliweza kukutana na wajumbe wa tume hiyo kwa sababu inavyoonekana serikali ndio inaandaa mipango yote kwa maana ya kwamba wanatumia magari ya serikali na kila kitu. Kwa hiyo walikutana nao wenyewe na baadaye tukakutana nao sisi kama mashirika na tukawaeleza ukweli. Tuliwaambia hali halisi na ukweli ambao tunaujua, zaidi walituuliza masuala ya Loliondo na tuliwaeleza jinsi ukiukwaji wa haki za binadamu ulivyofanyika."
Malengo ya ujio wa tume hio
Malengo mengine ya ujio wa tume hii ni pamoja na kupanua wigo wa mkataba wa Afrika juu ya haki za binadamu na watu, pamoja na mikataba mingine ya kikanda inayohusu haki za binadamu, kwa kubadilishana uzoefu na serikali ya Tanzania na baadhi ya wadau muhimu. Mwaka jana naibu waziri wa katiba na sheria wa Tanzania Godfrey Pinda, alikwenda mjini Banjul Gambia yalipo makao makuu ya tume ya Afrika ya haki za binadamu, na alinukuliwa akisema kuwa hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu hasa hasa haki za wa jamii ya wafugaji wa Masai wa Loliondo na Ngorongoro na hivyo tume imekuja kuthibitisha hilo.
Wakili Denisi Oulushangai anaongeza kwamba Hawatakutana na watu sahihi ambao ni wahanga wa oparesheni za serikali zilizofanyika mwezi juni mwaka 2022, ambapo zaidi ya watu 31 walijeruhiwa kwa risasi, na kuna mzee mmoja wa miaka 84amepotea na mpaka leo hajulikani alipo. Tunategemea kamisheni wafike kuonana na wahanga halisi.
Baada ya ziara hiyo, tume inatarajiwa kutoa taarifa kwa ufupi kwa mamlaka husika za jamhuri ya muungano wa Tanzania, pamoja na kufanya mkutano na waandishi wa habari, na baada ya hapo ripoti ya ziara nzima itawasilishwa mbele ya tume kwa ajili ya mapitio ili baadaye kuridhiwa kuwa ripoti ya tume kwenye vikao vitakavyofanyika siku za usoni.