Rais Samia akosowa mfumo wa utoaji haki
1 Februari 2023Rais Samia aliwaambia wanasheria waliokusanyika kuadhimisha Siku ya Sheria jijini Dodoma kwamba kasi ndogo ya mifumo ya utoaji haki inaongeza gharama na hata kuathiri mazingira ya uwekezaji na biashara katika nchi hiyo iliyo kwenye ukanda wa Afrika mashariki.
Kiongozi huyo wa Tanzania, ambaye amekuwa mara kwa mara akikemea hali isiyoridhisha kwenye taasisi za kiusalama na kisheria nchini mwake, ameziagiza mamlaka husika katika suala la utoaji haki kuhakikisha zinaweka nguvu kwenye tafiti za kuleta ufanisi katika utoaji haki, ikiwa ni pamoja na kutumia tafiti hizo katika kujiwekea mikakati ya muda mfupi, ya kati na muda mrefu kutekeleza matokeo yake kwendana na matarajio ya wananchi.
Kadhalika Rais Samia ameagiza kuchukuliwa hatua kwa watumishi ambao bado wanachafua sura na taswira ya muhimili wa mahakama nchini Tanzania kwa vitendo viovu vya rushwa, kauli mbaya pia vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalum.