Asasi za kiraia kutoridhishwa na tathmini kuhusu Loliondo
26 Januari 2023Katika barua yao, mashirika hayo nane yaliyopo Arusha kaskazini mwa Tanzania yamebainisha kwamba hayajaridhishwa na jinsi zoezi hilo lilivyofanyika kwani makamishina wa tume hiyo ya haki za binadamu Afrika yenye makao yake makuu mjini Banjul Gambia, hawakuwa huru kukutana na wahanga halisi, bali maafisa wa serikali ya Tanzania walikuwa nao bega kwa bega na kuwatafutia watu wa kukutana na kuzungumza nao.
Kulingana na barua hiyo, uwepo wa maofisa wa serikali wakati wa mahojiano na tume, pamoja na ratiba yao kutotoa nafasi ya kukutana na wanananchi na azaki, kulifanya azaki kusikilizwa kwa njia ya dharura kutegemeana na muda na ratiba iliyopangwa na serikali. Wakili Denis Olushangai ni mwakilishi wa mashirika hayo.
Kwa upande mwingie baadhi ya wakaazi wa tarafa ya Loliondo na Ngorongoro ambao ndio wanatajwa kuwa waathirika wakubwa wa uvunjifu wa haki za binadamu wanasema hawakupata nafasi yakutoa maoni yao na kwa jumla hawakuwa na taarifa za ujio wa tume hiyo.
Serikali yatupilia mbali madai ya uvunjifu wa haki
Pamoja na mambo mengine mashirika hayo pia yanashinikiza kuwekwa wazi kwa tarehe ambayo makamishina hao wa tume watazungumza na vyombo vya habari ili kutoa fursa kwa vyombo huru vya habari kuhudhuria.
Hata hivyo serikali ya Tanzania imekuwa ikikanusha vikali madai ya uvinjifu wa haki za binadamu katika maeneo hayo ambapo mwaka jana naibu waziri wa katiba na sheria wa Tanzania Godfrey Pinda, alikwenda mjini Banjul Gambia yalipo makao makuu ya tume ya Afrika ya haki za binadamu, na alinukuliwa akisema kuwa hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu hasa hasa haki za wa jamii ya wafugaji wa Masai wa Loliondo na Ngorongoro.