1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiKimataifa

Je, uhalifu wa kivita unapimwa vipi kwenye mzozo?

23 Oktoba 2023

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilitangaza kuwa, moja ya tume zake huru za uchunguzi tayari ilikuwa imekusanya "ushahidi uliyo wazi" wa uhalifu wa kivita uliofanywa na pande zote mbili.

https://p.dw.com/p/4XuAV
Makao Makuu ya Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICC
Makao Makuu ya Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICCPicha: Klaus Rainer Krieger/reportandum/IMAGO

Uhalifu wa kivita dhidi ya raia umefafanuliwa katika Kifungu cha 8 cha Mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na umetokana na Mikataba ya Geneva ya mwaka 1949.

Uhalifu huo unaelezwa kama ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu haswa ukiukaji dhidi ya raia wakati wa vita.

David Crane, mtaalam wa sheria za kimataifa kutoka Marekani akiwa pia mwendesha mashtaka mkuu na mwanzilishi wa Mahakama Maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu Sierra Leone, ameliambia Shirika la habari la Associated Press kwamba kuwalenga kwa makusudi raia na miundombinu ya kiraia bila sababu ya msingi ni uhalifu wa kivita.

Soma pia:UN yasema uhalifu wa kivita umeongezeka Myanmar

Na amesema hiyo ni sheria ambayo pande zote mbili zinapaswa kuizingatia kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Msingi wa kisheria wa "uhalifu wa kivita" ni tofauti na ule wa "uhalifu dhidi ya ubinadamu" au "mauaji ya kimbari."

Ingawa uhalifu wa kivita unahusu tu migogoro inayotokea ndani ya nchi au kati ya mataifa mawili,  uhalifu dhidi ya ubinadamu au mauaji ya kimbari vinaweza kutekelezwa hata wakati wa amani.

Mashambulizi ya raia huzingatiwa uhalifu wa kivita?

Kwa kifupi, hapana. Ni jibu lake Mark Kersten anayefuatilia masuala ya ulimwengu na Sera ya Umma katika Chuo Kikuu cha Toronto alipozungumza na DW mwaka 2022.

Kersten alisema sheria za vitasiku zote haziwalindi raia dhidi ya kifo na kwamba kila kifo cha raia hakiwezi moja kwa moja kuchukuliwa kama kinyume cha sheria.

Miundombinu ya kiraia ilioshambuliwa Kusini mwa Gaza
Miundombinu ya kiraia ilioshambuliwa Kusini mwa GazaPicha: Said Khatib/AFP

Uainishaji wa kitendo cha kijeshi wakati wa vita kama uhalifu wa kivita unategemea kama kitendo hicho kilihalalishwa.

Kwa hivyo ulipuaji wa shule au jengo la makazi hauwezi kuchukuliwa kuwa uhalifu wa kivita ikiwa ingechukuliwa kuwa muhimu kijeshi.

Ugumu wa kutofautisha hii tayari umedhihirika katika mzozo wa sasa.

Gaza, moja ya maeneo yenye watu wengi zaidi duniani, ambapo baadhi ya wataalamu wanasema haiwezekani kushambulia eneo hilo bila kuwaua miongoni mwa raia wapatao milioni 2.2 ambao wanaishi huko.

Soma pia:Pande hasimu zimefanya uhalifu wa kivita Sudan

Katika hali kama hii, ni muhimu kulenga vyema eneo la shambulio na kubaini iwapo uhalifu wa kivita ulitendeka.

Mahakama maalumndizo huamua kama kitendo fulani cha kijeshi ni uhalifu wa kivita kwa kutumia kanuni tatu:

kutofautisha, uwiano na tahadhari. Uwiano unalipiga marufuku jeshi kujibu mashambulizi kwa kutumia vurugu kupita kiasi.

Suala la kutofautisha linawataka wanajeshi kujaribu mara kwa mara kutofautisha kati ya raia na wapiganaji.

Na pia tahadhari inahitajika kadri iwezekanavyo ili kuepuka kuwadhuru raia. Licha ya yote hayo, bado ni vigumu mno kufafanua kwa uwazi uhalifu wa kivita.

Jukumu la Mahakama ya  ICC ni lipi?

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi ndiyo mahakama pekee ya kudumu ya kimataifa yenye mamlaka ya kufuatilia mashitaka ya uhalifu wa kivita, uhalifu wa kimataifa wa mauaji ya halaiki pamoja na uhalifu dhidi ya binadamu.

Amnesty: Urusi imefanya uhalifu Ukraine

Mahakama hiyo ilianzishwa mnamo 2002 kwa mujibu wa Mkataba wa Roma.

Nchi zote zilizosaini mkataba huo zina wajibu wa kushirikiana na ICC na kutii sheria fulani kama vile kutoa uwezo wa kuwafikia mashuhuda na vielelezo muhimu, lakini pia kuwakamata watu walioshtakiwa. 

Soma pia:Amnesty Inernational: Pande zinazozozana Sudan zatenda uhalifu wa kivita

ICC iliitambua Palestina kama nchi mwanachama mwaka 2015. Hata hivyo Israel, Marekani, China, Urusi na Misri si wanachama wa Mahakama hiyo.

Kwa hivyo ingawa ICC ina mamlaka yakubainisha uhalifu wa kivita katika mzozo uliopo huko Gaza, maamuzi yake hayatokuwa na mamlaka yoyote kwa Israel.

ICC imekuwa pia ikikabiliwa na wakati mgumu  wa kushtaki uhalifu wa kivita hata ulipofanywa na nchi ambazo ni sehemu ya Mkataba wa Roma.

ICC imefanikiwa kutoa hukumu chache tu katika miongo miwili tangu kuundwa kwake.