1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Mshukiwa wa mauaji ya kimbari Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Daniel Gakuba
25 Mei 2023

Mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Fulgence Kayishema, amekamatwa nchini Afrika Kusini. Haya yamesemwa Alhamisi na kitengo cha Umoja wa Mataifa cha kuchunguza uhalifu wa kivita uliofanywa nchini Rwanda.

https://p.dw.com/p/4RoHz
Fulgence Kayishema
Picha: UN IRMCT

Kulingana na kitengo hicho Kayishema anatuhumiwa kupanga mauaji ya karibu Watutsi elfu 2 wengi wao wakiwa watoto na wanawake waliokuwa wamepata hifadhi katika Kanisa Katoliki la Nyange wakati wa mauaji hayo ya kimbari ya mwaka 1994.

Tangu mwaka 2001, Kayishema alitoweka na alikuwa hajulikani alipo. Taarifa zinasema mamlaka za Afrika Kusini zilisaidia katika kukamatwa kwa polisi huyo wa zamani wa mahakama.

''Jana (Jumatano) jioni, mmoja wa wahalifu wanaotafutwa sana duniani, Flugence Kayishema alitiwa mbaroni katika mji wa Paarl nchini Afrika Kusini, kwa operesheni ya pamoja na Afrika Kusini,'' imesema taarifa ya kitengo cha mahakama ya kimataifa kinachoshughulikia mashitaka ya mauaji ya kimbari, MICT.

Kayishema anakabiliwa na mashitaka ya kufanya mauaji ya kimbari, kula njama ya kufanya mauaji ya kimbari pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Mshukiwa huyo aliyezaliwa mwaka 1961, amekuwa akijificha tangu Julai 2001.

Watu zaidi ya 800,000 waliuawa kinyama katika muda wa siku 100 nchini Rwanda mwaka 1994, wengi wao wakiwa kutoka jamii ya Watutsi. Wauwaji walikuwa Wahutu wenye misimamo mikali ya ukabila.