1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaanzisha uchunguzi kwa mapigano ya Sudan

14 Julai 2023

Mwendesha Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Jinai ya The Hague- (ICC), Karim Khan amesema kwa wakati huu mahakama imeanzisha uchunguzi mpya kuhusu madai ya uhalifu wa kivita nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/4TtQ2
Guinea Conakry | Beginn Prozess 2009 Stadion-Massaker | Karim Khan, Internationaler Strafgerichtshof
Picha: Souleymane Camara/REUTERS

Khan ametoa tangazo hilo katika ripoti yake mahususi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikiwa ni takribani miezi mitatu baada ya makabiliano makali baina ya majenerali wa jeshi wa taifa hilo la kaskazini/mashariki mwa Afrika kutumbukia katika machafuko.

Katika taarifa yake hiyo Khan amesema kumekuwa na mkururo wa mawasiliano yenye kujikita katika suala la uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu tangu kuzuka kwa mapigano nchini Sudan mwezi Aprili.

ICC yabainisha mateso ya wengi Sudan.

Mbele ya baraza hilo, mwendesha mashataka huyo amsema na hapa namnukuu: "Katika kipindi hiki ambacho tunazungumza, kuna wanawake, watoto wa kiume na wa kike, vijana na wazee wanaoishi kwa mashaka kutokana na mapigano hayo."

Südsudan Rubkona County | Flüchtlinge
Wanawake, watoto na wazee wakiwa katika wakati mgumu kufuatia mapigano nchini SudanPicha: Isaac Mugabi/DW

Anasema makaazi yao yamechomwa moto, huku wengi wao hawajui hatma yao na hatari itakayoweza kuwafika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeupokea vyema uchunguzi huo ikisema utatuma ujumbe kwa wale wote wanaofanya vitendo viovu huko Sudan na maeneo mengine. Katika taarifa yake msemaji wa wizara hiyo, Matthew Miller anasema uhalifu wa namna hiyo ni kinyume na utu.

Changamoto ya wachunguzi wa kimatiafa.

Hata kabla ya kuzuka kwa mapigano ya hivi karibuni, katikaa ripoti yake Khan ameonesha  kuzorota kwa mahusiano baina ya Sudan na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa.

Mkutano wa kilele wa mataifa jirani na Sudan,uliofanyika Alhamis mjini Cairo, Misri, ulihimiza kusitishwa mapigano nchini humo, lakini vita viliendelea  na kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ufaransa-AFP likinukuu wakazi katika baadhi ya maeneo linasema ndege za kivita kwa mara nyingine zilifanya mashambulizi karibu na mji mkuu wa Khartoum.

ICC imekuwa ikifanya uchunguzi katika jimbo la Darfur, hukohuko Sudan tangu 2005 baada ya mahakama hiyo kumtuhumu aliyekuwa rais wa taifa hilo kiongozi wa kiimla Omar al-Bashir kwa mashtaka kadhaa yakiwemo ya mauwaji ya watu wengi.

Soma zaidi:UN: Watu 87 walikwa katika kaburi la pamoja Darfur

Takribani watu 3,000 wameuwawa na wengine milioni tatu wameachwa bila ya makaazi tangu kutokea kwa machafuko baina ya mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan na aliyekuwa naibu wake Mohammed Hamdan Daglo anaekiongoza kikosi cha kukabiliana na matukio ya dharura (RSF)

Chanzo: AFP