ICC yaanzisha uchunguzi mpya katika machafuko ya Sudan
14 Julai 2023Mwendesha mashitaka mkuu Karim Khan ametoa tangazo hilo katika ripoti aliyowasilisha kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baada ya miezi mitatu ya vita kati ya majenerali wawili wanaozozana kuitumbukiza nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika katika machafuko.
ICC imekuwa ikichunguza uhalifu katika jimbo la Darfur nchini Sudan tangu mwaka wa 2005 baada ya agizo la Baraza la Usalama, na mahakama hiyo yenye makao makuu yake mjini The Hague imemfungulia mashitaka aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Omar al-Bashir, kwa makosa yakiwemo mauaji ya kimbari.
Karibu watu 3,000 wameuawa na wengine milioni tatu wameyakimbia makaazi tangu machafuko yalipozuka kati ya mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, na wanamgambo wa RSF wa aliyekuwa naibu wake, Mohamed Hamdan Dagalo.