1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJapan

Japan, Marekani kuunda mfumo kuzuia makombora masafa marefu

Hawa Bihoga
14 Agosti 2023

Japan na Marekani zinatarajiwa kwa pamoja kutengeneza mfumo wa kisasa, utakaonasa na kuzuia makombora ya masafa marefu. Hatua hiyo inafanyika huku hali ya wasiwasi ikizidi kuongezeka katika rasi ya Korea.

https://p.dw.com/p/4V95q
Japan Tokio | US-Verteidigungsminister Lloyd Austin und Premierminister Fumio Kishida
Picha: Eugene Hoshiko/AFP/Getty Images

Makubaliano ya kuanza kutengenezwa kwa mfumo huo yanatarajiwa kufanyika wakati waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida atakapofanya ziara nchini Marekani iliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa.

Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu Fumio Kishida na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol, katika mkutano wa kilele wa Usalama wa pande tatu, ambao utafanyika katika kambi ya David karibu na mji wa Washington siku ya Ijumaa.

Mkutano huo wa washirika hao watatu unatarajiwa kujikita kuiangazia Korea Kaskazini na mpango wake wa mara kwa mara wa majaribio ya makombora ya masafa marefu unaozidi kushamiri na kuongezeka kwa ushawishi wa China katika kanda hiyo.

Soma pia:Marekani, Japan na Korea Kusini zalaani hatua ya Korea Kaskazini kurusha kombora

Waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida alisema zaidi ya hayo, wanataraji kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo kuhusu masuala kama vile kukabiliana na Korea Kaskazini.

"Kudumisha na kuimarisha utaratibu huru na wazi wa kimataifa unaozingatiautawala wa  sheria." Alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Wasiwasi wa hali ya usalama katika kanda

Mzozo kwenye rasi ya Korea katika siku za hivi karibuni unazidi kufukuta huku Korea Kaskazini ikizindua awamu nyingine ya majaribio ya urushaji wa makombora ya masafa marefu.

Maazimio ya Umoja wa Mataifa yanapiga marufuku nchi iliyojitenga kimataifa kufanya majaribio ya makombora ya masafa yoyote.

Korea Kaskazini yafyatua tena makombora

Mifumo hiyo ambayo pia ni silaha aina ya Hypersonic inamilikiwa pia na China na Urusi na ambayo pia Korea Kaskazini imetangaza kutengeneza, ni ngumu zaidi kuizuia kulingana na mfumo wake wa kisasa na utendaji kazi maduhubuti na kasi katika kupangua mashambulizi.

Kulingana na muundo wao, makombora kama hayo yanaweza pia kuwa na kichwa cha nyuklia.

Korea Kaskazini pia inadai kufanya majaribio ya makombora hayo ya kasi aina ya hypersonic,na kuruhusu kile kinachoitwa ndege nyepesi ambayo imeundwa kuruka kwa muda mrefu bila kutumia injini, kutoka kwenye makombora ya masafa marefu.

Soma pia:Korea Kaskazini yafanya jaribio la kombora la masafa marefu

Chini ya mikakati mipya iliyotolewa mwezi wa Desemba, serikali ya Kishida inaahidi kujenga jeshi kubwa lenye uwezo wa kushambulia na kuongeza zaidi bajeti katika sekta ya ulinzi.

Japan, Marekani na Korea Kusinizimekubali kuanza kupeana taarifa muhimu, ikiwemo kuhusu urushwaji wa makombora ya Korea Kaskazini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Baada ya tangazo la mkutano huo lililotolewa na Ikulu ya Marekani White house, Balozi wa Marekani nchini Japan Rahm Emanuel kupitia mtandao wa twitter alisema kwamba, mkutano wa washirika hao watatu utakuwa ni wa kihistoria wenye matokeo ya mabadiliko ya kimkakati kidhana.