Japan itaharibu kombora litakalorushwa na Korea Kaskazini
29 Mei 2023Korea Kaskazini imesema imekamilisha satelaiti yake ya kwanza ya kijeshi ya ujasusi na tayari kiongozi wake Kim Jong Un ameidhinisha maandalizi ya mwisho ya kuipeleka angani.
Waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida tayari ameziagiza mamlaka husika kukusanya na kuchambua taarifa za kijasusi na kuongeza hatua kama hizo zinakiuka sheria za kimataifa.
"Matumizi ya teknolojia ya makombora ya nyuklia yatakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na yanaweza kuibua kitisho kikubwa na wasiwasi wa usalama kwa watu wa Japan.", alisema Kishida.
Kishida aidha amesema anashirikiana kwa karibu na Marekani na Korea Kusini, huku akiiomba Pyongyang kuachana na hatua hiyo.
Wachambuzi wanasema satelaiti ya kijeshi inaweza ikaimarisha uwezo wa Korea Kaskazini wa kijasusi na kushambulia maeneo inayoyalenga kunapotokea vita.