1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran yaapa kuchukua hatua kujibu vikwazo vipya

11 Septemba 2024

Marekani na mataifa yenye nguvu ya Magharibi, yametangaza vikwazo vipya kwa Iran kwa sababu ya kuipa Urusi makombora ya masafa mafupi kwa ajili ya mashambulizi yake dhidi ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4kVBg
Iran Teheran | Rais Masoud Pezeshkian
Rais wa Iran Masoud PezeshkianPicha: Iranian Presidency/ZUMA Press Wire/picture alliance

Marekani imetangaza vikwazo vipya kuwalenga watu 10 na kampuni sita katika nchi za Iran na Urusi kujibu kile ilichokiita uamuzi uliopitiliza wa Iran wa kupeleka makombora ya masafa mafupi nchini Urusi, katika jibu la pamoja na washirika wake wa Ulaya.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia imeliwekea vikwazo shirika la ndege la Iran kwa kujihusisha katika uchumi wa Urusi kwenye sekta ya usafirishaji, kulingana na taarifa ya Wizara ya Hazina ya Marekani.

Katika mkutano na waandishi wa habari huko mjini London, kabla ya Blinken na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy, kufanya ziara nchini Ukraine, Blinken amesema Marekani imeionya Iran kwa faragha juu ya hatua yake ya kuipa Urusi makombora ya masafa mafupi.

Ukraine US-Außenminister Antony Blinken und britische Außenminister David Lammy
Kushoto: Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken(kulia)Picha: Mark Schiefelbein/picture alliance/AP

Soma Pia:  Kiongozi wa Iran afunguwa mlango wa mazungumzo na Marekani kuhusu Nyuklia

Kwa upande wake Iran imekanusha kwamba imeipelekea Urusi silaha. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kanaani, aliandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa hizo ni propaganda na taarifa za kupotosha za nchi za Magharibi kwa lengo la kufunika hatua za Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi za kupeleka msaada mkubwa wa silaha za kijeshi kwa Israel ambazo zinasababisha mauaji katika Ukanda wa Gaza. Iran imesema itachukua hatua kujibu vikwazo hivyo vipya vya nchi za Magharibi.

Katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika Septemba 10, maafisa wakuu na wanadiplomasia walitoa wito wa kusitishwa kwa vita nchini Ukraine, wakitaja umuhimu wa kushughulikia mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka kila uchao na kuendelea kuteseka kwa raia.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pia zimetangaza vikwazo vipya kwa Iran na Urusi, zimesema upelekaji wa makombora Urusi ni tishio la moja kwa moja kwa Usalama wa Ulaya.

Iran Tehran | IRGC | Kombora la masafa mafupi Tondar-69
Kombora la masafa mafupi aina ya Tondar-69 la IranPicha: Sobhan Farajvan/Pacific Press/picture alliance

Vikwazo hivyo ni pamoja na kufutwa kwa mikataba ya huduma za safari za ndege kati ya nchi hizo na Iran, ambavyo vitalizuia shirika la ndege la Iran kufanya safari nchini Uingereza na pia katika nchi zingine za barani Ulaya.

Iran tayari ni mojawapo ya nchi zilizowekewa vikwazo vikali duniani, na baadhi ya wataalam wamehoji athari za kuiongezea adhabu za kiuchumi ambazo zinaweza kuwaumiza zaidi watu wa kipato cha kati kuliko viongozi wa nchi hiyo.

Soma Pia: Masoud Pezeshkian: Nini cha kutarajia kutoka kwa rais mpya wa Iran 

Wakati huo huo, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ameanza ziara yake nchini Iraq, akilenga kuimarisha uhusiano wa karibu na nchi hiyo jirani katika safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu aingie madarakani.

Waziri Mkuu wa Iraq, Mohamed Shia al-Sudani alimkaribisha kiongozi huyo wa Iran alipowasili mjini Baghdad.