AfD cha Ujerumani kutajwa kama kundi la itikadi kali?
12 Machi 2024Kwa miaka mingi, chama hicho cha kisiasa Mbadala kwa Ujerumani, AfD na idara hiyo ya upelelezi wa ndani, BfV, yenye jukumu la kuilinda katiba, wamekuwa wakipambana mara kadhaa mahakamani, na hoja kubwa ikiwa ni kama BfV ina uwezo wa kisheria wa kukichunguza chama kinachoshukiwa kufanya shughuli zinazokinzana na katiba.
Mnyukano wa sasa wa kisheria unashuhudiwa katika Mahakama ya Juu zaidi ya Kiutawala, OVG iliyoko mjini Münster mnamo kuanzia Machi 12 hadi 13.
Soma pia:Mahakama Ujerumani yapiga marufuku chama cha itikadi kali cha Heimat kupokea ruzuku ya serikali
AfD inapinga uamuzi uliotolewa mwaka 2021 ulioagiza chama hicho kuchunguzwa kutokana na madai ya kuwa na itikadi kali za mrengo wa kulia na hasa kutokana na misimamo yake mikali iliyoibua mashaka.
Wakati huo, idara hiyo ya upelelezi ingeweza kuchukua hatua zaidi kuliko taasisi yoyote ile kwa kuzingatia machapisho kwenye magazeti, mitandaoni, ripoti zilizorushwa kwenye vituo vya televisheni na kwenye intaneti, kusikiliza hotuba zilizotolewa na wanachama wa AfD bungeni na hata kwenye makongamano ya chama hicho na kuyatumia.
Ikiwa rufaa ya AfD itafanikiwa, basi chama hicho hakitachunguzwa zaidi.
Wakati huo huo, BfV inakusudia kwenda mbali zaidi kwa kukiainisha chama cha AfD kama kundi la "mrengo wa kulia wenye msimamo mkali" katika ngazi ya shirikisho, badala ya kuliacha kuwa suala la kuchunguzwa kwa muda mrefu ili kuthibitisha ukweli.
Mjadala juu ya kukizuia chama cha AfD
Hivi sasa wanachama waliothibitishwa kama wenye misimamo mikali huenda wakafuatiliwa zaidi na idara za upelelezi kuliko wakati wowote ule.
Soma pia: Hofu ya "fashisti" kuongoza serikali ya jimbo Ujerumani
Na ikiwa AfD itashindwa kwenye rufaa hii, huenda shinikizo la kukipiga marufuku chama hicho likaanza. BfV, tayari imeainisha mahitaji maalumu ikiwa shinikizo hilo litaanzishwa, ikiwa ni pamoja na kuweko vielelezo thabiti vinavyothibitisha kwamba chama hicho kina lengo la kushambulia na kuuondoa utaratibu wa uhuru na wa kidemokrasia wa nchini Ujerumani.
AfD kunyimwa fedha za kodi?
Kisheria, ni Mahakama ya Katiba ya Shirikisho inayotakiwa kutoa uamuzi wa ikiwa chama kinaweza kupigwa marufuku au la. Ombi la zuio linaweza kuwasilishwa na serikali ya shirikisho, Bundestag ama Bundesrat.
Muungano wa vyama tawala katika jimbo la Bremen vya Social Democrats, SPD, Kijani na cha Kushoto unajiandaa kuchukua hatua hiyo.
Soma pia: AfD yaongoza dhidi ya CDU jimboni Saxony kuelekea uchaguzi wa Septemba
Hata hivyo, Wajerumani wengi wana mashaka: Kwa mfano utafiti wa taasisi ya Infratest.dimap kwa mwaka huu wa 2024, asilimia 51 hawaungi mkono chama hicho kupigwa marufuku.
Lakini namna nyingine ya kudhoofisha uthabiti wa chama hicho itakuwa ni kukiondolea stahiki ya kupata ufadhili kutoka serikalini. Ufadhili huu ndio chanzo kikubwa cha mapato kwa vyama vingi, ukiachilia mbali ada na michango ya wanachama.
Na hata ikiwa hili litawezekana, swali ambalo bado linasalia miongoni mwa wafuatiliaji wa mambo ni kama hata kuna huo uwezekano wa kukipiga marufuku chama hicho.
Sikiliza zaidi: