1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umaarufu wa AfD wapungua kufuatia maandamano Ujerumani

23 Januari 2024

Uungwaji mkono wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Ujerumani Alternative für Deutschland, AfD, umeshuka kidogo katika utafiti wa maoni uliofanywa mara mbili hivi karibuni na uliochapishwa Jumanne.

https://p.dw.com/p/4bax1
Vijana mjini Berlin wakiandamana baada ya mkutano wa siri wa AfD huko Potsdam
Waandamanaji wakibeba bango la kukipinga chama cha AfDPicha: Christian Ditsch/epd/IMAGO

Hii inafuatia siku kumi za maandamano ya nchi nzima ya kukipinga chama hicho. Lakini chama hicho kimesalia katika nafasi ya pili katika vyama vyenye umaarufu zaidi nchini Ujerumani.

Utafiti wa maoni wa kila wiki uliofanywa na shirika la utafiti wa maoni la INSA kwa ajili ya gazeti la Ujerumani la Bild na iliyotolewa leo inaonyesha kuwa, uungwaji mkono wa chama cha AfD umeshuka kutoka asilimia 23 wiki iliyopita hadi asilimia 21.5.

Utafiti mwingine tofauti wa maoni uliofanywa na shirika la Forsa kwa ajili ya shirika la habari la RTL/ntv unaonyesha kwamba umaarufu wa chama hicho umeshuka kwa asilimia mbili hadi asilimia 20. Licha ya kushuka kidogo, umaarufu wa chama hicho umekuwa ukiongezeka kila panapofanywa kura za maoni tangu katikati ya mwaka 2022.

Chama cha Kansela Scholz chazidi kuporomoka

Tafiti zote mbili za maoni zimeonyesha kwamba muunganowa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union CDU na chama ndugu cha Christian Social Union CSU, kinasalia kuwa chama chenye umaarufu mkubwa Ujerumani kikiwa na asilimia 30.5, hiyo ikiwa ni katika utafiti wa maoni ya gazeti la Bild na utafiti wa RTL/ntv unaonyesha umaarufu wake ni wa asilimia 31.

Potsdam Kansela Scholz katika maandamano ya kupinga siasa za mrengo wa kulia
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Umaarufu wa chama cha Kansela Olaf Scholz cha Social Democratic SPD umeendelea kushuka na sasa umefikia asilimia 13.5 katika kura ya gazeti la Bild na asilimia 14 katika kura ya RTL/ntv, huku chama cha Kijani kikiungwa mkono na asilimia 12.5 na asilimia 14 katika kila kura ya mashirika hayo mawili ya habari.

Chama cha AfD hivi karibuni kimekuwa kikilengwa na maandamano ya kupinga siasa kali za mrengo wa kulia, yaliyowavutia zaidi ya watu milioni moja mwishoni mwa wiki iliyopita katika miji mingi kote Ujerumani.

Maandamano hayo yanafuatia ufichuzi kwamba wanachama wa chama hicho walihudhuria mkutano wa siri huko Potsdam mwezi Novemba, ulioweka mikakati ya kuwafukuza wahamiaji wakiwemo baadhi wenye uraia wa Ujerumani.

Vyama vya siasa kali havistahili kupata ufadhili

Hayo yakiarifiwa, Mahakama ya Katiba ya Ujerumani leo imesema serikali sasa inaweza kusitisha ufadhili wa chama cha mrengo wa kulia cha Die Heimat.

Deutschland Bundesministerin für Inneres und Heimat Nancy Faeser
Waziri wa usalama wa ndani Ujerumani Nancy FaeserPicha: Christophe Gateau/dpa/picture alliance

Uamuzi huo ambao ndio wa kwanza wa kivyake kutolewa Ujerumanidhidi ya chama cha kisiasa, umetolewa na mahakama ya Karlsruhe, iliyosema ufadhili wa chama hicho usitishwe kwa kipindi cha miaka sita kwa kuwa kinalenga kuhujumu au kuuondoa kabisa mfumo wa demokrasia Ujerumani.

Bunge la Ujerumani, Bundestag na baraza la juu la bunge la Ujerumani, Bundesrat pamoja na serikali, waliwasilisha kesi katika mahakama hiyo mwaka 2019 wakitaka kutolewe amri ya kusitishwa ufadhili wa chama hicho, kufuatia mabadiliko ya sheria ya kimsingi ya Ujerumani kwamba vyama vya siasa kali visipate ufadhili wa serikali ambao unatolewa kwa vyama vyengine.

Waziri wa usalama wa ndani wa Ujerumani, Nancy Faeser amesema uamuzi huo umetuma ishara ya wazi kwa wale wanaopinga demokrasia.

Vyanzo: DPAE/Reuters