Hofu ya "fashisti" kuongoza serikali ya jimbo Ujerumani
16 Januari 2024Kufichuliwa mwezi huu kwa mipango ya siri ya wanasiasa kutoka chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD) na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia kuwafukuza wahamiaji kumesababisha ongezeko la wataalamu wa siasa na manusura wa mauaji ya Holocaust kupendekeza kukipiga marufuku chama hicho kwa madai kuwa kimekuwa na itikadi kali.
Baada ya miaka kadhaa katika upinzani, wanachama wa AfD wenyewe wanaamini kuwa chama hicho kinakaribia kupata mafanikio. Kulingana na kura za maoni, kinatazamiwa kupata mafanikio makubwa katika chaguzi za mitaa, majimbo na Bunge la Ulaya.
Huko Ujerumani mashariki, chama hicho kiko mbele ya wapinzani wake, kikiwa na umaarufu wa zaidi ya asilimia 30. Wanachama wa AfD wameweka macho yao juu ya uwaziri mkuu wa jimbo dogo la Thuringia mnamo 2024. mgombea waliye naye akilini, Björn Höcke, ni mwenye msimamo mkali hasa.
Höcke, mwenyekiti wa kundi la wabunge wa AfD katika bunge la jimbo, ni mwalimu wa zamani wa shule ya upili na hapo awali aliandamana pamoja na Wanazi mamboleo.
Katika barua ya 2015, Bodi ya Utendaji ya AfD ilimshutumu Höcke kwa kuchapisha maandishi chini ya jina la uwongo "Landolf Ladig" ambayo "yalikuwa karibu sana na Ujamaa wa Kitaifa." Höcke alikanusha kuwa alifanya hivyo, lakini alikataa kutia saini hati ya kiapo inayosema hivyo.
Mnamo 2017, AfD ilijaribu kumfukuza Höcke bila mafanikio. Kamati ya Utendaji ya Shirikisho ilianza mchakato wa kumfukuza uanachama kufuatia hotuba yake yenye utata katika hafla ya chama huko Dresden ambapo alikosoa ukumbusho wa Ujerumani wa mauaji ya Holocaust.
Soma pia: AfD yaongoza dhidi ya CDU jimboni Saxony kuelekea uchaguzi wa Septemba
Aliutaja Ukumbusho wa Wayahudi Waliouawa wa Ulaya mjini Berlin kuwa "mnara wa aibu" na akaongeza: "Siasa hizi za kijinga za kukabiliana na siku za nyuma zinatulemaza - hatuhitaji chochote isipokuwa mabadiliko ya digrii 180 kwenye siasa za ukumbusho." Mahakama ya Usuluhishi ya Thuringian ilikataa kufukuzwa kwake.
Tangu wakati huo, chama kimekuwa na msimamo mkali zaidi na kinawiana zaidi na misimamo ya Höcke. Wafuasi wake wanaunda jukwaa la chama.
Kukuwa kwa mrengo wa kulia Ujerumani
Tangu utawala wa mauaji wa Ujamaa wa Kitaifa chini ya Adolf Hitler kutoka 1933 hadi 1945, maombi yoyote ya kiitikadi au ishara ya maadili ya Kinazi yamezingatiwa kuwa haramu nchini Ujerumani. Wakati wa enzi ya Wanazi, Wajerumani waliwaua Wayahudi zaidi ya milioni sita na walihusika na mzozo mbaya zaidi katika historia ya ulimwengu, Vita vya Pili vya Ulimwengu.
Leo, takwimu nyingi za AfD zimevutia nadhari kwa kauli zinazokumbusha Ujamaa wa Kitaifa. Mnamo 2019, mahakama ya Ujerumani iliamua kwamba Björn Höcke anaweza kuelezewa kisheria kama "fashisti," kulingana na "msingi wa kweli unaoweza kuthibitishwa."
Sasa, Höcke anaweza kuwa mwanasiasa wa kwanza wa mrengo mkali wa kulia katika Ujerumani baada ya vita kuchaguliwa kuwa mkuu wa serikali katika mojawapo ya majimbo 16 ya shirikisho. Ofisi hiyo ina mamlaka makubwa ya kisiasa: Wakuu wa Serikali kwa kiasi kikubwa wanawajibika kwa sera ya elimu na vyombo vya habari vya jimbo lao na wanaamua kuhusu maelezo ya utekelezaji wa sera ya hifadhi ya serikali ya shirikisho. AfD kwa muda mrefu imekuwa ikitoa wito wa mabadiliko makubwa bila shaka katika sheria za hifadhi na uhamiaji.
Mashambulizi dhidi ya vyombo vya habri vya umma
Katika mkutano wa AfD mwezi Novemba, Höcke aliahidi hatua kubwa iwapo atachaguliwa. Akasema: Tutasimamisha vita dhidi ya mrengo wa kulia! - na alishangiliwa na wafuasi. Höcke pia anataka kufanya mabadiliko makubwa kwa vyombo vya habari vya umma: "Ni nini kitatokea ikiwa Höcke atakuwa waziri mkuu wa jimbo? Je, atafuta mikataba ya vyombo vya habari vya serikali? Ndiyo, hivyo ndivyo Höcke atakavyofanya! Ndiyo!” alipiga kelele na kushangiliwa zaidi na wanachama wake wa AfD.
Baada ya miaka kadhaa ya ripoti za ukosoaji, AfD imetoa wito wa kukomeshwa au kuyafanyiwa marekebisho mashirika ya utangazaji ya umma nchini Ujerumani. Kwa msukumo wa Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, AfD inategemea kile kinachoitwa "vyombo vya habari mbadala" na kueneza sera zake kupitia chaneli zake za chama zinazofikia mbali kwenye mitandao ya kijamii.
Mnamo Desemba, tovuti ya uchambuzi wa kisheria ya Verfassungsblog (Blogu ya Katiba) ilieleza jinsi hali halisi ya waziri mkuu wa AfD inavyoweza kuwa.
soma pia: AfD kuamua wagombea wake katika bunge la Ulaya
Kulingana na uchambuzi wake, afisi isiyo na hadhi kubwa sana ya rais wa bunge la jimbo inaweza kuwa muhimu. Nchini Ujerumani, nafasi hiyo kawaida huenda kwa chama kilichofanikiwa zaidi katika chaguzi za majimbo. Na huko Thuringia, AfD iko mbele kwa uwazi katika kura za maoni. Hii ina maana kwamba ina nafasi halali ya kushinda ofisi hii.
"Uharibifu ambao chama cha kimabavu kinachoshikilia afisi hii kinaweza kufanya kwa demokrasia kwa jumla ni mkubwa," Verfassungsblog ilionya. Hii ni kwa sababu rais wa bunge la jimbo hupanga taratibu za bunge.
Ikiwa AfD ingeibuka kama chama chenye nguvu zaidi huko Thuringia kama ilivyotabiriwa - na takriban asilimia 35 ya kura, wabunge wanaweza kumweka Björn Höcke mbele kama mgombea wao wa mkuu wa serikali.
Huenda Höcke atashindwa kupata uungwaji mkono zaidi ya asilimia 50 katika awamu mbili za kwanza za upigaji kura ikiwa vyama vingine vyote vitapiga kura dhidi yake. Lakini, katika duru ya tatu ya upigaji kura, wingi mdogo tu wa kura utatosha.
Tumaini pekee kwa vyama vingine lingekuwa kuweka tofauti zao kando na kuungana katika muungano usio wa kawaida kutaja mgombea wa pamoja. Kwa ajili hiyo, vyama vya CDU na SPD vitalazimika kufanya kazi pamoja baada ya miaka mingi ya uchungu na mizozo ambayo imezikumba siasa za jimbo laThuringia.
Hakuna marufuku ya AfD - lakini marufuku ya Höcke?
Mnamo Januari 2024, wanaharakati wanaopinga mrengo wa kulia waliwasilisha ombi la kuitaka serikali ya Ujerumani kuwasilisha ombi katika Mahakama ya Kikatiba ya Shirikisho la kuondoa haki fulani za kimsingi za kiongozi huyo wa AfD wa Thuringian.
Hii ingezuwia uhuru wake wa kujieleza au uhuru wa kukusanyika. Mahakama inaweza pia kubatilisha haki yake ya kupiga kura na haki ya kuchaguliwa - na uwezo wa kushikilia ofisi ya umma. Ikiwa mgombeaji wake mkuu Björn Höcke ataathiriwa, AfD jimboni Thuringia inaweza kuathirika pakubwa.