Zelensky: Vikosi ya Ukraine vyapiga hatua dhidi ya adui
22 Mei 2024Katika hotuba yake kwa taifa Jumanne jioni, Zelensky amesema vikosi vya nchi hiyo katika eneo la Kharkiv,vinaendelea kupata ufanisi dhidi ya adui lakini akaonya hali upande wa mashariki karibu na miji ya Pokrovsk, Kramatorsk na Kurakhove imesalia kuwa "ngumu sana". Zelensky ameongeza kusema mapigano zaidi yanaendelea katika eneo hilo.
Soma pia:Zelensky anatarajia Urusi itaimarisha mashambulizi yake upande wa kaskazini
Wiki iliyopita, Rais huyo wa Ukraine alionya kwamba uvamizi wa Urusi Kharkiv huenda ukawa wimbi la kwanza na huenda vikosi vya Urusi vinalenga mji wa Kharkhiv, wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine.
Kuleba asema washirika wanaweza kudungua makombora ya Urusi
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, amesema Jumanne kwamba washirika wa nchi hiyo wanaweza kudungua makombora ya Urusi kutoka maeneo yao katika kile kilichoonekana kuwa ombi linalotokana a na ukosefu mkubwa wa mifumo ya ulinzi wa anga nchini humo.
Wakati wa mkutano na waandishi habari akiwa na mwenzake wa Ujerumani Annalena Baerbock aliyeko nchini humo kwa ziara yake ya nane tangu uvamizi wa Urusi, Kuleba alisema hakuna changamoto ya kisheria, kiusalama au ya kimaadili ambayo inazuia washirika wao kudungua makombora ya Urusi kwenye eneo la Ukraine kutoka maeneo yao.
Kwa upande wake, Baerbock amesema kuchelewesha msaada kwa Ukraine pia kunahatarisha usalama wa mataifa ya magharibi.
Mazungumzo ya kujiunga kwa Ukraine na Moldova EU yatarajiwa kuanza
Baada ya mkutano wa baraza la mawaziri Jumanne jioni mjini Brussels nchini Ubelgiji, waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Hadja Lahbib alisema Ukraine na Moldova zinaweza kutarajia kuanza haraka kwa mazungumzo ya kuwa wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Lahbib hakusema iwapo mataifa hayo yametimiza masharti yote ya kujiunga na Umoja huo ila tu kwamba yanaendelea na mchakato wa marekebisho.
Mawaziri wa fedha wa G7 kujadiliana kuhusu mali ya Urusi iliyofungiwa
Mawaziri wa fedha wa kundi la nchi tajiri kiviwanda G7 watakaokutana Italia wiki hii watajaribu kupata msimamo wa pamoja kuhusu namna ya kutumia mali ya Urusi iliyofungiwa kusaidia juhudi za Ukrainekatika vita vyake na nchi hiyo.
Mawaziri hao watakutana katika mji wa Stresa siku ya Ijumaa na Jumamosi.