1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Zelensky: Urusi itaimarisha mashambulizi yake mjini Kharkiv

Sylvia Mwehozi
21 Mei 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema anatarajia Urusi itaimarisha mashambulizi yake upande wa Kaskazini Mashariki na kuonya kwamba Kyiv imesalia na robo tu ya mifumo ya ulinzi wa anga kuweza kujilinda.

https://p.dw.com/p/4g5AG
Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Gints Ivuskans/AFP

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema anatarajia Urusi itaimarisha mashambulizi yake upande wa Kaskazini Mashariki na kuonya kwamba Kyiv imesalia na robo tu ya mifumo ya ulinzi wa anga kuweza kujilinda. Zelensky ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na shirika la habari la AFP.

Soma: Marekani yatangaza kitita kipya cha msaada kwa Ukraine

Vikosi vya Urusi ambavyo vimepata mafanikio ya wastani katika miezi ya hivi karibuni, vilifanya shambulizi la kushutukiza katika mkoa wa Kharkiv mnamo Mei 10 na kuchukua udhibiti mkubwa wa maeneo.

Zelensky amelieleza shirika la AFP, kwamba vikosi vya Urusi vilifanikiwa kusonga mbele kati ya kilometa 5 hadi 10 kuelekea mpaka wa kaskazini mashariki kabla ya kurejeshwa nyuma na vikosi vya Ukraine. Hata hivyo ameongeza kuwa mkoa huo unaweza kuwa wa kwanza katika wimbi la mashambulizi mapana ya Urusi.