Wajumbe wa ANC kumchagua kiongozi
16 Desemba 2022Takriban wajumbe 4,500 wa chama tawala cha ANC kutoka kote nchini Afrika Kusini wanatarajiwa kupiga kura wakati wa kongamano la siku tano linalofanyika karibu na mji wa Johannesburg.
Kashfa ya ufisadi inayomzunguka Ramaphosa, mizozo ndani ya chama hicho ni miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kutawala mkutano huo.
Soma pia: Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa asema atautetea wadhfa wake kisasa na kisheria
Ramaphosa anawania kushika tena hatamu za uongozi wa chama hicho tawala katika wakati ambapo chama hicho maarufu nchini Afrika Kusini kinakabiliwa na mipasuko na kupungua kwa uungwaji mkono wa umma baada ya miaka 28 madarakani.
Akijinadi kama mpambanaji wa ufisadi, Ramaphosa alichukua uongozi wa ANC mnamo mwaka 2017 kufuatia kashfa zilizomuandama Rais wa zamani Jacob Zuma.
Chama hicho cha ANC chenye wingi wa viti bungeni kina nguvu ya kumuidhinisha kiongozi wa taifa.
Hata hivyo, sifa za Ramaphosa zimetiwa doa na kugubikwa na madai ya ufisadi.
Ramaphosa anakabiliwa na shutma za ufisadi
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 70 anakabaliwa na shutma kuwa alificha wizi wa fedha katika shamba lake badala ya kuripoti uhalifu huo katika mamlaka husika.
Licha ya madai hayo mazito, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa njia ni nyeupe kwa Ramaphosa kuchukua uongozi wa chama hicho kufuatia uchaguzi wa wajumbe unaotarajiwa kufanyika Jumamosi.
Mwandishi wa habari za siasa nchini humo Ralph Mathekga ameeleza, "ANC inamuhitaji Ramaphosa. Atashinda. Hata wale wanaomchukia pia wanahitaji ashinde."
Nje ya ukumbi huo wa mkutano uliopambwa kwa rangi za kijani, manjano na nyeusi- ambazo ni rangi za chama hicho, kundi la wajumbe waliimba nyimbo kwa lugha ya Kizulu wakimtaka Ramaphosa ajiuzulu kutokana na kashfa hiyo ya shamba. Wajumbe hao pia waliimbia nyimbo za kumsifu Rais wa zamani Jacob Zuma.
Soma pia: Afrika Kusini kupewa milioni €600 kufanikisha nishati safi
Mchambuzi wa siasa nchini Afrika Kusini Moeletsi Mbeki amesema. "ANC inatumia muda mwingi kupigana wenyewe kwa wenyewe, badala ya kuleta utulivu wa taifa, hakuna mtu mwenye suluhu inayofanya kazi, kila mtu anamkaba koo mwenzake. Hali hiyo inazidisha hali ya kukataa tamaa kwa ANC miongoni mwa wapiga kura."
Kwa upande mwengine, kuelekea kongamano hilo la wajumbe wa ANC, Zuma ametangaza kumshtaki Ramaphosa kutokana na ripoti ya matibabu iliyovuja na inayohusishwa na kesi ya rushwa ya silaha ya miaka ya 1990.
Hata hivyo, kesi hiyo inatajwa kuwa haiwezi kuwa kikwazo kwa Ramaphosa kuchaguliwa kwa muhula wa pili kama kiongozi wa ANC. Ushindi wake utapiga muhuri wa kumkatia tiketi ya kuwa Rais baada ya uchaguzi wa mwaka 2024, iwapo chama chake kitashinda kura hiyo.