Afrika Kusini: Rais Ramaphosa asema hang'atuki ng'o.
4 Desemba 2022Kwa mujibu wa msemaji wake rais huyo anayekabiliwa na kashfa na kitisho cha kuondolewa madarakani hana nia ya kujiuzulu na kwamba ataendelea kupambana kisiasa na kwa njia za kisheria.
Ramaphosa amekuwa akikabiliwa na shutuma tangu mwezi Juni, baada ya mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi alipowasilisha malalamiko kwa polisi akidai kuwa rais huyo hakuripoti polisi wizi uliotokea mwezi Februari mwaka 2020 katika shamba lake kaskazini mashariki mwa nchi. Katika malalamiko hayo Ramaphosa pia anadaiwa kuwa alipanga juu ya kutekwa nyara wezi hao na kisha kuwahonga ili wanyamaze kimya.
Soma Zaidi:Rais Ramaphosa akabiliwa na shinikizo la kujiuzulu
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amekana kufanya makosa yoyote lakini kashfa dhidi yake na taarifa za kupatikana zaidi ya dola nusu milioni zilizofichwa kwenye mito ya makochi, zimetolewa wakati mbaya kwake kutokana na kwamba mnamo Desemba 16, Ramaphosa atagombea kwenye uchaguzi wa rais wa chama tawala cha ANC nafasi ambayo ni muhimu katika kumwezesha kuendelea kusalia kama rais wa taifa la Afrika Kusini.
Msemaji wa rais bwana Vincent Mangwenya ameeleza kwamba Rais Ramaphosa anatilia maanani ujumbe kutoka kwenye matawi ya chama tawala ambayo yamemteua kugombea muhula wa pili wa uongozi wa chama cha ANC na kwamba Rais ramaphosa anaelewa kuwa ujumbe huo unamaanisha kwamba unamtaka aendelee kuongoza ili afanikishe mageuzi ya serikali na kiuchumi.
Mangwenya ameongeza kusema kwamba Ramaphosa kwa unyenyekevu na kwa uangalifu mkubwa na kujitolea kwake amekubali wito huo wa kuendelea kukihudumia chama chake cha ANC na kwa watu wa Afrika Kusini.
Soma Zaidi:Hatima ya kisiasa wa rais Ramaphosa iko matatani
Viongozi wa kamati ya chama tawala nchini Afrika Kusini wanatarjiwa kuamua siku ya Jumapili iwapo wataendelea kumuunga mkono Rais Cyril Ramaphosa.
Siku ya Ijumaa kamati hiyo kuu ya ANC ilifanya mazungumzo baada ya jopo la bunge kutoa ripoti iliyoashiria kupatikana ushahidi wa awali kuhusu kutendekea utovu wa nidhamu na kwamba huenda rais Ramaphosa alikiuka sheria za nchi. Ripoti hiyo itapelekwa bungeni siku ya Jumanne na hoja inaweza kuwasilishwa ya kupigwa kura ya kumwondoa madarakani Ramaphosa.
Kikao kiliamua nini
Mweka Hazina Mkuu wa ANC, Paul Mashatile aliviambia vyombo vya habari kuwa katika kikao hicho kifupi iliamuliwa kuwa ripoti hiyo ishughulikiwe kwanza na viongozi wakuu wa chama kabla ya kamati kuu kukutana tena siku ya Jumapili. Rais Ramaphosa hakuhudhuria mkutano wa Ijumaa.
Vyombo vya habari vya Afrika Kusini vimeendelea kuonesha imani kwamba Ramaphosa atasalia madarakanimkwa kuwa anapendwa na umma.
Chama cha ANC cha shujaa wa taifa la Afrika Kusini Nelson Mandela, kimo madarakani kwa miaka 28 tangu kumalizika kwa ubaguzi wa rangi nchini humo, kinaendelea kupoteza uungwaji mkono.
Ramaphosa alichukua wadhifa wa kuliongoza taifa lililoendelea zaidi kiuchumi barani Afrika mnamo mwaka 2018, akiahidi kung'oa rushwa katika taasisi za serikali.
Chanzo: AFP