Vita nchini Kongo yaongeza mzozo wa afya ya akili
16 Oktoba 2024Makundi ya misaada yanasema idadi ya watu wanaohitaji huduma za afya imeongezeka mno wakati mapigano nayo yakishika kasi. Wengi wamekata tamaa, kiasi cha kutamani kujiua, wakidhani hiyo ndio namna ya kujipumzisha dhidi ya madhila yanayowakabili.
Nelly Shukuru, mwenye miaka 51, aliyeyakimbia makazi yake kutokana na mapigano, alijikuta njia panda, hata akatamani kujiua ili kuhitimisha madhila kuanzia ya vita, hali mbaya kwenye makambi ya wakimbizi wa ndani huko Mashariki mwa Kongo hadi njaa. Hakuwa na namna nyingine ya kuyaepuka.
Soma pia: Mashirika ya kiutu yadai Wakongo hawajafikiwa na misaada
Mwanamama huyu mwenye watoto sita aliyekuwa amekaa kwenye kituo cha afya, anasema, akili yake ilitawaliwa na mateso anayoyapitia na hata anaona ni heri kwa watu waliokufa, kuliko yeye aliye hai. Akaongeza kuwa, kama si jirani yake naye angekuwa marehemu.
Huduma za afya ya akili ni chache mno
Makundi ya misaada yanasema idadi ya watu wanaohitaji huduma za afya imeongezeka mno wakati mapigano nayo yakishika kasi. Na kwa wale wanaoendelea kupona baada ya matibabu, wanaishi kwenye mazingira magumu sana na badala ya kuwapa matumaini ya kupona, pengine inazidi kuwakatisha tamaa.
Idadi ya watu waliopata usaidizi wa kisaikolojia katika kambi karibu na Goma iliongezeka zaidi ya asilimia 200 kati ya Januari na Juni ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023, ambayo ilikuwa kutoka watu 6,600 hadi zaidi ya 20,000, hii ikiwa ni kulingana na kikundi cha misaada cha Action Against Hunger.
Na hata idadi ya watu wanaoripoti kutamani kujiua imeongezeka kutoka karibu tano kwa mwezi mwanzoni mwa mwaka hadi zaidi ya 120.
Eneo la mashariki mwa Kongo limekuwa likizozaniwa na wanamgambo
Zaidi ya makundi 100 ya wanamgambo yamekuwa yakiliwania eneo la mashariki ya Kongo, karibu na mpaka na Rwanda ambalo lina hifadhi kubwa ya madini. Mapigano yamesambaa, na hasa baada ya kundi la waasi la M23 likiibuka upya. Zaidi ya watu 600,000 wanaishi kwenye makambi karibu na mji wa Goma.
Innocent Ntamuheza, Mtaalamu wa saikolojia kwenye kundi hilo anasema watu wanaoishi kwenye makambi hayo, wanakumbwa na wasiwasi, huzuni na kiwewe, lakini pia msongo wa mawazo pamoja na kukosa usingizi. Wengine wanakunywa pombe kupita kiasi na kutumia dawa za kulevya.
Lakini ni bahati mbaya kwamba, watu hawa wanapata msaada kiduchu wa kisaikolojia. Na hii kwa sababu ufadhili wa huduma hizo ni mdogo mno.
Shukuru, anasema alitaka kujiua mnamo mwezi Agosti baada ya kijana wake mwenye miaka 21 kumpiga na jiwe kichwani, kisa, walikuwa wakigombania radio.
Lakini pia watoto wake pia wamekuwa ni walevi wa kupindukia tangu walipofika kambini kwa sababu hawana cha kufanya, anasema Shukuru. Walikuwa wakiishi katika mji wa Sake ambako walikuwa wakilima na kwenda kanisani. Lakini walikimbia mwezi Februari kutokana na mshambulizi ya mabomu.
Na mumewe, ambaye ni fundi ujenzi anapambana kutafuta ajira kwa kuwa misaada wanayoipata haiwatoshelezi.
Serikali ikisaidiwa na makundi mengine ya wanamgambo wanaojiita Wazalendo wanajaribu kuwafurusha M23. Lakini kwa upande mwingine wanashutumiwa kwa kukiuka haki za binaadamu na unyanyasaji wa kingono.
Mwanamke mmoja wa miaka 38 alisema alibakwa na wanamgambo watatu huko mashambani alipokuwa akitafuta chakula mnamo mwezi Mei. Mama huyu wa watoto watatu anayetibiwa na Madaktari Wasio na Mipaka, MSF anasema kila akilala huwa anawaona wanaume hao. Kwake yeye haoni umuhimu wa wanajeshi kuwa karibu nao.
Watoto waathirika kwa kutenganishwa na wazazi wao
MSF ilisema mwezi Septemba kwamba ilitibu idadi ambayo haijawahi kushuhudiwa ya waathirika wa ukatili wa kijinsia nchini Kongo mwaka uliopita. Zaidi ya 25,000, na hali hii inaendelea.
Lakini wale waliotibiwa wanasema imewasaidia kujifunza njia za kukabiliana na wasiwasi na mawazo mabaya.
Shirika la War Child linalowasaidia watoto kwenye mizozo limesema watoto wanaoathirika zaidi ni wale waliopoteza wazazi wao kutokana na kifo ama kutenganishwa.
Novemba mwaka jana, mtoto wa miaka 14 alitenganishwa na familia yake wakati
mji wao uliposhambuliwa. Ingawa analelewa na familia nyingine, lakini ana wasiwas wa kushambuliwa. Sasa anafikiria kujiua ili kukomesha mateso.
Hajui kama mama yake yuko hai na msaada anaopewa anasema humsaidia kwa muda tu.
Soma pia: Milio ya mabomu yarindima karibu na Goma, DR Congo