1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yaishitaki Rwanda kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki

1 Oktoba 2024

Chini ya wiki moja baada ya kufungua kesi kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki dhidi ya Rwanda, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema ina imani ya kutendewa haki na mahakama hiyo ya kikanda.

https://p.dw.com/p/4lIVE
DR Kongo | Félix Tshisekedi
Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: DW

Mnamo tarehe 26 Septemba, serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilifunguwa kesi kwenye Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye makao yake makuu mjinii Arusha kaskazini mwa Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne (Oktoba 1), Naibu Waziri wa Sheria wa Kongo ,Samuel Mbemba, alisema nchi yake ilikuwa na imani na Mahakama hiyo na kwamba aliamini kwamba Kongo ingelitendewa haki.

Soma zaidi: DRC imekua rasmi mwanachama wa saba wa EAC

Mbemba aliwaambia waandishi hao mjini Kinshasa kwamba nchi yake iko katika vita vitatu, ambavyo ni vya kijeshi, vya kidiplomasia na vya kisheria, lakini kwa kuwa "majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki hawaegemei upande wowote ule" alisema hakuwa na wasiwasi.

Akijibu swali kuhusu kwa nini Kongo, ambayo haikuwa na imani na majeshi ya Jumuiya Afrika Mashariki, inatangaza kuwa na imani na mahakama ya Jumuiya hiyo, Mbemba alisema kesi hiyo ingelichukuliwa kwa busara ya kisheria.

"Majaji kwenye mahakama ya nchi ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wanafahamu kwamba ujio wa mahakama hiyo na watu kuwa na imani nayo kutatokana na kesi hii. Lakini kwa siku ya kwanza ya kesi kusikilizwa, tulitambuwa ya kwamba majaji wako huru na mahakama iko huru na imara kwenye lengo lake." Aliongeza Mbemba.

Mashirika ya kiraia yatoa sauti

Nayo mashirika ya kutetea haki za binaadamu ambayo kila uchao yanalalamikia madhambi wanayotendewa Wakongomani na vita vya kila siku vilivyodumu kwa zaidi ya miongo mitatu sasa.

Rwanda Paul Kagame
Rais Paul Kagame wa Rwanda.Picha: Presidency Of Rwanda/Anadolu/picture alliance

"Itakuwa afueni kwa Kongo, ikiwa Rwanda itahukumiwa pale, lakini nina mashaka hasa kuhusu uwezo na mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu nchi na sio watu," alisema Angélus Kavuthirwaki wa asasi za kijamii.

Soma zaidi: Mahakama Kongo yawahukumu kifo watu 37 waliojaribu mapinduzi

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Vijana wa Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini, mwanasheria Trésor Katoto, alisema kumekuwa na vitendo vibaya sana ambavyo raia wamekuwa wahanga, na kwamba "hukumu itakayotolewa na mahakama ya Arusha, itakuwa hukumu stahiki."

Tangu kumalizika kwa vita vya Agosti 1998, serikali ya Kongo imekuwa ikiilaumu Rwanda kuivamia ardhi yake kupitia makundi mbalimbali ya uasi. 

Awali lilikuwa kundi la CNDP la Jenerali Laurent Nkunda, baadaye ikaja M23 iliyoongozwa na Bishop Runiga, na kwa sasa ni AFC-M23 inayoongozwa na Coreneille Nangaa.

John Kanyunyu/DW Goma