Mapigano yaongezeka mashariki ya Kongo
29 Juni 2024Makabiliano ya jana Ijumaa yalitokea katika mji wa Kanyabayonga, ulioko kaskazini mwa uwanja wa mapambano katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Mkoa huo umekumbwa na machafuko tangu mwaka wa 2021 wakati M23 walipoanzisha tena harakati zao za mapigano katika eneo hilo.
Mji wa Kanyabayonga unazingatiwa kuwa mlango wa kuingia Butembo na Beni katika upande wa kaskazini, ambazo ni ngome za kabila la Nande na vituo muhimu vya kibiashara. Kanyabayonga, ni mji wenye wakazi 60,000, na uko karibu kilomizta 100 kutoka mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma, ambao pia umezingirwa na waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda.
Waasi wa M23 walisonga mbele kuelekea Kanyabayonga katika wilaya ya Lubero, ikiwa ni eneo la nne la mkoa huo, ambalo kundi hilo limeingia baada ya Rutshuru, Nyiragongo na Masisi. Afisa mmoja wa utawala katika eneo hilo amesema mapigano yanaendelea katika eneo la Kanyabayonga na viunga vyake, lakini jeshi bado liko huko.