Jeshi la Kongo latangaza kuzima jaribio la waasi wa M23
31 Mei 2024Mizinga na aina nyingine za kombora zilitumiwa na pande zote mbili, huku jeshi la serikali likivurumisha mabomu kuelekea ngome za waasi kutokea Mugunga kando na kambi za wakimbizi mjini Goma.
Taarifa zinaeleza kuwa makombora yalilenga vijiji vya Vunano pamoja na kilima kinachokaliwa na waasi cha Kihuli kilicho umbali wa kilomita 4 kutokea mji wa Sake.
Barabara inayotoka Sake kuelekea mji wa Mushaki imefungwa kufuatia mashambulizi hayo.
Maroketi yaharibu makazi katika mlima Macha
Guillaume NJIKE, ambaye ni msemaji wa gavana mkoani Kivu Kaskazini amesema "Mapema asubuhi hii Alhamisi wanajeshi wa FARDC walijibu ipasavyo uchokozi wa magaidi waliofyatua risasi ovyo ovyo katika mji wa Sake na kwenye maeneo yanayozunguka mji huo."
Soma pia:Waasi wa M23 wauteka mji wa madini wa Rubaya nchini Kongo
Hata hivyo, majibu ya waasi kwa shambulizi hilo yalikuwa ni mabaya zaidi baada ya kurusha maroketi kuelekea mji wa Sake ambako idadi ndogo ya raia walikuwa wamekwama katika nyumba zao.
Ripoti zinasema kuwa maroketi hayo yaliangukia nyumba za raia kwenye mlima wa Macha katikati mwa mji huo na kusababisha maafa mengi, yakiwemo uharibifu mkubwa wa magari ya kikosi cha SADC.
Wakaazi wahofia usalama, wakimbia makazi yao
Wakaazi wa Goma na wa Sake wameonekana kuanza kuyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi yaliyoshuhudiwa.
"Tunaogopa lakini hadi sasa hatujui tutakwenda wapi. Mji wa Goma upo karibu na hapa Sake. Waasi wa M23 walishachukuwa Masisi, Rutshuru...kwa hiyo tukikimbilia Goma inamaanisha kwamba sote tutakimbilia ziwani," alisema mmoja ya wakazi hao.
Wakati huo huo, kwenye mkanda wa video uliozunguka mtandaoni jana usiku, mamia wa raia wa mji mdogo wa Kanyabayonga wilayani Lubero walionekana wakikimbia nyumba zao.
Duru zisizoegemea upande wowote zimefahamisha kuwa waasi wa M23 wamepiga kambi moja iliyo umbali wa kilomita nne na mji huo huku idadi ndogo ya vijana Wazalendo wakiendelea kushika doria baada ya jeshi kuondoka.
Soma pia: Bomu laua watu 12 wakiwemo watoto nchini Kongo
Vyanzo hivyo vimeeleza pia kuwa magari ya jeshi la serikali yalionekana yakiondoka kwenye mji huo unaopakana na vijiji vinavyokumbwa na vita katika wilaya jirani ya Rutshuru.
Mji huo ulioko umbali wa kilometa 175 kutoka Goma uliwapokea tangu mwanzoni mwa mwezi huu zaidi ya wakimbizi Elfu 30 ambao sasa wameanza tena kukimbia.