Madrid: Viongozi waadhimisha siku ya kupambana na ukame
17 Juni 2022Ibarahim Thiaw, katibu mtendaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na kuenea kwa majangwa au UNCCD, amesema wakati wa ufunguzi wa mkutano huo kwamba madhara ya ukame yanaweza kuathiri hadi theluthi mbili ya wanadamu ifikapo mwaka 2050. Na kwamba hakutakuwa mahali pa kujificha ikiwa tutashindwa au tutapuuza kuzuia uharibifu mkubwa tunayofanya kwenye sayari dunia. Hivyo ni lazima tuwe tayari kukabili hali halisi iliyoko sasa.
Mkutano huo unaandaliwa kuadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na kuenea kwa jangwa, uharibifu wa misitu na ukame.
Thiaw amesema nusu ya idadi jumla ya watu ulimwenguni inatarajiwa kukumbwa na uhaba mkubwa wa maji katika miaka minane ijayo.
Ameongeza kuwa hali kama hiyo inaweza kuwaweka takriban watu milioni 700 au asilimia 10 ya idadi jumla ya watu ulimwenguni kuwa katika hatari ya kuyakimbia makwao katika kipindi hicho.
Wataalam kadhaa wameuhudhuria mkutano huo, miongoni mwao ni Mkenya Patricia Kombo, ambaye ni mwanzilishi wa mradi wa kupanda miti PaTree. Anawashirikisha wanafunzi kupanda miti kama sehemu ya juhudi za kuisaidia Kenya kuhakikisha asilimia 10 ya ardhi yake ni misitu.
''Ninajua wengi wenu mlioko hapa hamjakumbana na ukame, lakini ningependa kuwaambia jinsi ukame ulivyo. Kupata maji safi na salama ya kunywa ni sawa na kupata almasi. Kuweza kula mara tatu kwa siku huwa ndoto ya mchana,'' Kombo aliwaambia waliohudhuria mkutano huo.
Aliongeza kuwa jamii zimegeukia machafuko kwa sababu ya ukosefu wa chakula na maji. "Unapigana kusudi ukipate kile kidogo kilichoko. Tunapigania maji.
Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez pia aliuhutubia mkutano huo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitarajiwa kutoa hotuba yake kwa njia ya video.
UNCCD inasema kati ya mwaka 1900 na 2019, ukame umewaathiri watu bilioni 2.7 duniani na umesababisha vifo milioni 11.7.
Wizara ya Mpito ya Ekolojia ya Uhispania inasema asilimia 75 ya ardhi ya Uhispania ipo katika hatari ya kupoteza miti na misitu yake, na hali hiyo inazidi kuongezeka.
Mkutano huo umejiri mnamo wakati Uhispania inakumbwa na joto kali lisilo la kawaida ambalo limechangia ongezeko la visa vya moto sehemu mbalimbali nchini humo.
Dhamira ya mkutano huo ni kuhimiza hatua za mapema kuchukuliwa kuzuia majanga na madhara mabaya kutokea siku za baadaye.
(APE)