1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Viongozi wa nchi wanachama wa SCO waahidi kushikamana

4 Julai 2024

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai SCO wameendelea na mazungumzo yao katika mkutano wa kilele unaofanyika Kazakhstan.

https://p.dw.com/p/4hsRZ
Mkutano wa SCO huko Astana - Marais Vladimir Putin na Xi Jinping
Rais wa Urusi Vladimir Putin (kushoto) akisalimiana na rais wa China Xi Jinping mjini Astana; KazakhstanPicha: Sergei Guneev/Pool/Sputnik/REUTERS

Pembezoni mwa mkutano huo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai  SCO unaoendelea huko mjini Astana, miongoni mwa nchi zilizoahidi kusuluhisha tofauti zao ni India na China kufuatia mvutano wao kuhusu eneo pana linalojumisha sehemu ya safu za milima la Himalaya.

Mvutano kati ya Beijing na New Delhi umeendelea tangu kuliposhuhudiwa makabiliano ya mwezi Juni mwaka 2020 kwenye eneo hilo la mpakani linalozozaniwa na mataifa hayo mawili, ambapo askari walipigana kwa mawe, marungu na ngumi na kupelekea vifo vya angalau wanajeshi 20 wa India na wanne wa China.

Soma pia: Putin, Xi kwenye mkutano wa Ushirikiano wa Shanghai

Waziri wa mambo ya nje wa India Subrahmanyam Jaishankar amekutana na mwenzake wa China Wang Yi leo Alhamisi huko Kazakhstan na wawili hao wameafikiana kuendeleza mazungumzo ya kusuluhisha suala hilo na kusisitiza kuwa kuongezeka kwa hali ya sasa ya mvutano katika eneo hilo hakuna maslahi yoyote kwa nchi hizo.

Waziri wa mambo ya nje wa India Subrahmanyam Jaishankar
Waziri wa mambo ya nje wa India Subrahmanyam JaishankarPicha: Johannes Simon/Getty Images

Kwa upande mwingine, Ikulu ya Kremlin imesema hii leo kuwa Waziri Mkuu wa India Narendra Modi atafanya ziara nchini Urusi mnamo Julai 8-9 na kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin.

Urusi na India zimeimarisha mahusiano yao na New Delhi imekuwa mshirika mkuu wa biashara wa Moscow. Kwa sasa, China na India ni wanunuzi wakuu wa mafuta ya Urusi kufuatia vikwazo vilivyowekwa na Marekani na washirika wake wa Magharibi kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Soma pia: Waziri Mkuu wa India Modi aelekea Moscow, Vienna wiki ijayo

Naye Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan alizungumza na mwenzake wa China Xi Jinping na kumueleza umuhimu wa kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili. Viongozi hao walijadili pia vita vya Urusi nchini Ukraine na mapigano huko Gaza, huku Erdogan akisisitiza kuwepo kwa "hatua madhubuti" za  jumuiya ya kimataifa ili kuzuia kutanuka kwa migogoro hiyo.

Umoja wa Mataifa wawatolea wito viongozi wa SCO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Picha: Luiz Rampelotto/EuropaNewswire/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipohutubia mkutano huo, amezihimiza nchi wanachama wa SCO kuchukua hatua kuhusu hali ya mizozo inayoendelea ulimwenguni pamoja na kitisho cha mabadiliko ya hali ya hewa.

"Tunakutana katikati mwa hali ngumu ulimwenguni: vita vinavyoendelea, mifarakano ya ya kikanda, janga la kutowawajibisha wahusika wa maovu, kurudi nyuma kwa malengo ya Maendeleo Endelevu, unyama na migogoro ya kutoaminiana. Kwa bahati mbaya, watu wanaanza kupoteza imani katika ushirikiano wa kimataifa. Wanataja ahadi zilizovunjwa, undumilakuwili na ukosefu mkubwa wa usawa. Changamoto hizi za kimataifa haziwezi kutatuliwa na kila nchi kivyake. Huu ni wakati wa kuthibitisha dhamira yetu ya pamoja ya kuunga mkono malengo ya ushirikiano wa pande zote."

Lakini viongozi wa Urusi na China ambao ndio walioanzisha Jumuiya hiyo ya Ushirikiano wa Shanghai SCO  mnamo mwaka 2001, wamezitolea wito nchi wanachama kuimarisha mifumo ya usalama, kuwepo kwa ushirikiano wa dhati wa kisiasa pamoja na ushirikiano wa kiuchumi ili kukabiliana ipasavyo na miungano na ushawishi wa mataifa ya Magharibi.

(Vyanzo: Mashirika)