Putin, Xi kwenye mkutano wa Ushirikiano wa Shanghai
3 Julai 2024China na Urusi zimeimarisha ushirikiano wao na zinataka kuongeza ushawishi wao ili kuzipiku nchi za Magharibi katika eneo la kimkakati la Asia ya Kati.
Rais wa Urusi Vladimir Putin, amewasili katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana Jumatano asubuhi kwa ajili ya mkutano huo wa kilele wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO) ambayo ni kambi ya kikanda inayoongozwa na China.
Shirika hilo linazijumuisha nchi za Asia ya Kati, India na Iran.
Moscow na Beijing zimeimarisha uhusiano wao wa kisiasa, wa kijeshi na kiuchumi tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake nchini Ukraine mnamo Februari, 2022.
Pamoja na kiongozi wa China Xi Jinping, ambaye aliwasili Kazakhstan siku ya Jumanne, nchi hizo mbili washirika China na Urusi wanauona ushirikiano wa SCO kama jukwaa muhimu la kuendeleza maslahi yao ya kimkakati katika maeneo yote yanayojumuisha mabara ya Ulaya na Asia.
Soma Pia: Dubai, Kazakhstan na Urusi zashuhudia mafuriko makubwa
Vyombo vya Habari vya serikali ya China vimesema Rais Xi Jinping, anaunga mkono Kazakhstan kujiunga na muungano wa BRICS, wakati ambapo kundi la mataifa wanachama wa jumuiya hiyo yanafikiria kuongeza wanachama zaidi ili kushindana na nchi za Magharibi ambazo wanasema utaratibu wao wa mfumo wa dunia umepitwa na wakati.
Shirika la Ushirikiano la Shanghai, (SCO) lilianzishwa mwaka 2001 na China na Urusi kufuatilia na kujadili masuala ya usalama katika nchi za Asia ya Kati na eneo pana katika kanda hiyo.
Soma Pia: Viongozi wa SCO wasifia maendeleo ya jumuiya yao
Wanachama wengine wa (SCO), ni Iran, India, Pakistan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Uzbekistan. Nchi washirika wa Ushirikiano huo wa Shanghai ni pamoja na Uturuki, Saudi Arabia na Misri.
Alexander Gabuev, mkurugenzi wa Kituo cha Eurasia cha Carnegie cha nchini Urusi amesema mkutano wa mwaka huu unahudhuriwa na, mbali na marais Putin na Xi, na mwenyeji wa mkutano huo wa kilele Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev.
Viongozi wengine ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, ambaye anatembelea Asia ya Kati, Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif, Marais Shavkat Mirziyoyev wa Uzbekistan, Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Ilham Aliyev wa Azerbaijan.
Wengine ni Marais Emomali Rakhmon wa Tajikistan, Sadyr Zhaparov wa Kyrgyzstan na Rais wa Belarus Alexander Lukashenko ambaye nchi yake inakuwa mwanachama kamili wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO).
Iran itawakilishwa na kaimu Rais Mohammad Mokhbar.
Vyanzo:AFP/RTRE