1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wapendekeza suluhisho la amani kwa mzozo wa Ukraine

17 Juni 2024

Viongozi wa dunia waliunga mkono uhuru wa Ukraine na ulinzi wa ardhi yake, katika siku ya mwisho ya mkutano wa kilele wa amani nchini Uswisi.

https://p.dw.com/p/4h82d
Mkutano wa amani wa Ukraine nchini Uswisi
Viongozi wa dunia wakikusanyika katika mkutano wa amani wa Ukraine nchini Uswisi: 15.06.2024Picha: EPA/MICHAEL BUHOLZER

Viongozi hao walijadili namna ya kumaliza vita kati Moscow na Kiev pamoja na hitaji la kufanya mazungumzo na Urusi, lakini wakashindwa kuelezea ni jinsi gani na lini hilo litafanyika.

Zaidi ya miaka miwili baada ya Urusi kuivamia Ukraine, viongozi na maafisa wakuu kutoka zaidi ya nchi 90 walijadiliana kwa siku mbili mwishoni mwa juma katika eneo la mapumziko lenye milima huko  Burgenstock nchini Uswisi ili kujaribu kutafuta  suluhu ya mzozo mkubwa zaidi barani Ulaya tangu kumalizika Vita vya pili vya Dunia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alipongeza "mafanikio" ya kidiplomasia ya mkutano huo ambao Urusi haikualikwa. Mazungumzo ya Jumamosi na Jumapili yanatoa fursa ya kuandaliwa mkutano wa pili wa amani, wenye dhamira ya kupatikana kwa suluhu ya haki na ya kudumu ili kuvimaliza vita hivyo.

Rais Zelensky akihutubia mkutano huo wa amani nchini Uswisi
Rais Zelensky akihutubia mkutano huo wa amani nchini UswisiPicha: Sean Kilpatrick/Zumapress/IMAGO

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi na uongozi wake hawako tayari kwa amani ya haki.

Aidha Moscow, imezidisha harakati zake za kijeshi kwa lengo la kuudhibiti mji mkuu Kyiv ambao itautumia kama shinikizo ili kuanzisha mazungumzo. Wiki iliyopita Urusi ilisema iko tayari kusitisha vita mara moja ikiwa Ukraine itaachana na azma yake ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kuondoa wanajeshi wake katika mikoa minne ya Ukraine iliyonyakuliwa na Urusi. Masharti ambayo Kiev iliyataja kuwa upuuzi mtupu.

Soma pia: Mkutano wa kilele wa Ukraine waanza Uswisi lakini huenda ukashindwa kuitenga Urusi

Leo hii, Mkuu wa idara ya ujasusi wa Urusi na mshirika wa karibu wa Putin Sergei Naryshkin asema ikiwa pendekezo la mkataba wa amani lililopendekezwa na Rais wa Urusi litakataliwa, basi masharti yajayo yatakuwa magumu zaidi.

Tamko la pamoja la mazungumzo hayo

Tamko la pamoja la mkutano huo, lililoungwa mkono na nchi nyingi zilizohudhuria linaeleza kuwa ili kufikia amani kunahitaji ushirikishwaji na mazungumzo kati ya pande zote, na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru na uhalali wa eneo la mataifa yote ikiwemo Ukraine, kwa kuzingatia mipaka inayotambuliwa kimataifa.

Uswisi - Mkutano wa kilele wa amani wa kujadili namna ya kumaliza vita vya Ukraine
Mkutano wa kilele wa amani wa kujadili namna ya kumaliza vita vya Ukraine uliofanyika Juni 15 na 16, 2024Picha: Michael Buholzer/REUTERS

Tamko hilo limeongeza kuwa tishio lolote au matumizi ya silaha za nyuklia katika vita havikubaliki, na usalama wa chakula ni lazima usitumiwe kama silaha ya vita, na kuhimiza zoezi la kubadilishana wafungwa wa vita na kurejeshwa nchini Ukraine kwa watoto wote waliohamishwa  na raia wanaozuiliwa kinyume cha sheria.

Soma pia: Mkutano wa kimataifa wa amani Ukraine wafungua Uswisi

Lakini baadhi ya mataifa yaliyohudhuria mkutano huo kama India, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu hayakuunga mkono tamko hilo. Wachambuzi wametilia shaka mafanikio ya mkutano huo kwanza kutokana na tofauti zilizopo baina ya nchi washiriki, kutoalikwa kwa Urusi na kususiwa na China. Baadhi wameeleza pia kwamba huenda  Kiev imeshindwa kufikia lengo lake la kuitenga Moscow.

Muda mchache uliopita, Ikulu ya Kremlin imesema matokeo ya mkutano huo yalikuwa ni sawa na sifuri na kudhihirisha kwamba mazungumzo yoyote bila kuishirikisha Urusi hayawezi kuwa na mafanikio yoyote. Lakini hadi sasa haijafahamika wazi ni lini, wapi na namna gani mazungumzo mengine ya amani yatafanyika na kuishirikisha Urusi.

(Vyanzo: Mashirika)