Utawala wa kijeshi waitisha maandamano makubwa Niger
3 Agosti 2023Wito huo wa maandamano ya kuunga mkono mapinduzi tayari umeitikiwa na mamia ya watu katika mji mkuu wa Niger Niamey, huku baadhi yao wakiwa na bendera kubwa za Urusi.
Waandamanaji hao wamekusanyika katika uwanja wa Uhuru katikati mwa jiji, kufuatia wito wa muungano wa vyama vya kiraia katika siku hii ya kuadhimisha uhuru wa nchi hiyo uliopatikana mwaka 1960 kutoka kwa Ufaransa.
Kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdourahmane Tchiani, amezikemea baadhi ya nchi jirani na jumuiya ya kimataifa na kutoa wito kwa raia wa Niger kuwa tayari kulilinda taifa.
" Raia wenzagu wa Niger, sherehe za uhuru wa Niger zinafanyika mwaka huu katika hali ya kipekee kufuatia mapinduzi ya Julai 26, 2023. Vikosi vya Ulinzi na Usalama vimechukua uongozi na hivyo kusitisha utawala wa awamu ya saba. Ni muhimu kusisitiza kwa uwazi kwamba sababu pekee ya hatua hii ni kuilinda nchi yetu ya Niger. "
Tchiani amesema Niger itakabiliwa na nyakati ngumu katika siku zijazo na kwamba misimamo "ya uadui mkali" ya wale wanaopinga utawala wake haina maana. Amesema vikwazo vilivyowekwa wiki iliyopita na Jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS ni haramu na vya kinyama.
Soma pia: Mtawala wa kijeshi Niger aonya dhidi ya uingiliaji wa kigeni na kuutaka umma kuilinda nchi
Mahaman Sanoussi, mratibu wa muda wa kikundi cha asasi za kiraia cha M62 amesema ni vyema kuendelea kuhamasisha raia na kwamba wanachokitaka ni kuondoka mara moja kwa vikosi vyote vya kigeni.
Shinikizo na Vikwazo vya ECOWAS
ECOWAS imetishia pia kutumia nguvu iwapo Rais Mohamed Bazoum, ambaye bado yuko chini ya kizuizi cha nyumbani hatoachiliwa huru na kurejeshwa madarakani kabla ya Agosti 6 mwaka huu. Rais wa Marekani Joe Biden ametoa pia wito hii leo wa kuachiliwa kwa Bazoum na kuilinda demokrasia ya Niger.
Ufaransa imeitaka serikali mpya ya Niger kuhakikisha kikamilifu usalama wa ubalozi wake huko Niamey pamoja na balozi za mataifa mengine ikisisitiza kuwa hilo ni jukumu lao chini ya sheria ya kimataifa, hasa Mkataba wa Vienna.
Tangu siku ya Jumanne wiki hii, Ufaransa tayari imewahamisha raia wake pamoja na watu wengine wapatao 1000. Hii leo pia, Marekani na Uingereza zimetangaza kuwaondoa wafanyakazi wa ubalozi wao nchini Niger kufuatia wasiwasi wa kiusalama kutokana na maandamano hayo.
Hayo yanajiri wakati wakuu wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS wanahitimisha hii leo mkutano wa siku mbili wa kujadili athari na hatua za mapinduzi ya serikali nchini Niger.