Mtawala wa kijeshi Niger aonya dhidi ya uingiliaji wa kigeni
3 Agosti 2023Katika moja ya hotuba chache kwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi tangu alipokamata madaraka kutoka kwa rais wa Niger aliyechaguliwa kidemokrasia wiki moja iliyopita, Tchiani ameonya dhidi ya uingiliaji wa kigeni na uingiliaji wa kijeshi nchini humo.
Amewatolea wito watu wa Niger kusimama pamoja na kuwashinda wale wanaotaka kusababisha mateso makubwa kwa raia wao wanaofanya kazi kwa bidii na kuidhoofisha nchi.
Soma pia:Rishi Sunak na Olaf Scholz walaani jaribio la mapinduzi Niger
Aidha ameahidi kutengeneza mazingira ya mpito wa amani kuelekea uchaguzi kufuatia hatua yake ya kumuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum.
Hotuba yake ya jana usiku iliyorushwa kwenye televisheni ilijiri wakati kukiwa na ongezeko la mvutano wa kikanda huku jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi - ECOWAS ikiitishia kutumia nguvu za kijeshi ikiwa Bazoum hatoachiliwa huru kutoka kifungo cha nyumbani na kurejeshwa madarakani ifikapo Agosti 6.