1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Ndege za kwanza kutoka Niger zatua Paris

2 Agosti 2023

Ndege mbili za kwanza zilizokuwa zinawabeba raia wa Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya walioondolewa kutoka Niger, zimetua mjini Paris Jumatano.

https://p.dw.com/p/4UgCP
Niger Französische Soldaten unterstützen französische Staatsangehörige auf einem Flugplatz
Watu waliokusanyika nje ya uwanja wa ndege wa Niamey wakisubiri kusafirisha ParisPicha: Sam Mednick/AP Photo/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo raia wa kigeni wamekusanyika mapema Jumatano nje ya uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Niger, Niamey wakisubiri ndege ya tatu itakayowarudisha makwao.

Ndege ya kwanza iliyowasili mjini Paris ilikuwa na zaidi ya watu 260 wakiwemo watoto 12. Sehemu kubwa walikuwa raia wa Ufaransa ila raia wa Niger, Ureno, Ubelgiji, Ethiopia na Lebanon walikuwa miongoni mwa waliokuwemo katika ndege hiyo pia.

Kulingana na gazeti la Ufaransa Le Parisien, wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imesema ndege ya pili ilikuwa imewabeba raia wa Ufaransa, Niger, Ujerumani, Ubelgiji, Canada, Marekani, Austria na India.

Suluhisho la kidiplomasia ndio muhimu

Mamlaka za nchini Italia zimesema pia kwamba zimewaondoa kutoka Niger karibu raia 100 wa kigeni wanaoishi Niger ambao wamewasili mjini Roma mapema leo, huku redio ya nchini Italia ANSA ikiripoti kwamba miongoni mwao walikuwa raia 36 wa Italia na Wamarekani 21.

Niger Französische Soldaten unterstützen französische Staatsangehörige auf einem Flugplatz
Raia wanaousibiri kuondolewa Niger kufuatia mapinduziPicha: Sam Mednick/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani ana matumaini kwamba suluhisho linaweza kupatikana katika huo mzozo wa Niger.

"Tutaona kitakachofanyika nchini humo. Narudia, sisi kawaida tunapenda suluhisho la kidiplomasia na ndio maana ubalozi wetu umesalia wazi na tutaona kitakachofanyika. Bila shaka tunataka demokrasia irudi ila cha muhimu ni kwamba tumewarudisha watu wetu wote waliotaka kurudi Italia na pia tumechangia kuwaondoa Afrika, wengi ambao si raia wa Italia," alisema Tajani.

Mamia ya watu wameonekana katika uwanja wa ndege wa Niamey mapema Jumatano wakisubiri kuondoka baada ya safari ya tatu ya ndege kufutiliwa mbali usiku wa kuamkia leo. Baadhi wamelala sakafuni huku wengine wakionekana wakicheza michezo ya video.

Mipaka yafunguliwa tena

Wakati huo huo, usiku wa kuamkia Jumatano, Niger imetangaza kwamba inafungua mipaka yake na majirani zake kadhaa, wiki moja baada ya mapinduzi ambayo yameitikisa kanda ya Sahel huko Afrika Magharibi.

Jumuiya ya Kimataifa yalaani mapinduzi nchini Niger

Jeshi liliifunga mipaka ya nchi hiyo Jumatano iliyopita mara tu baada ya kutangaza kwamba limemuondoa madarakani kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Bazoum.

Jumuiya ya Kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS imeweka vikwazo vikiwemo kusitisha miamala yote ya fedha na kuzifungia raslimali za kitaifa. Jumuiya hiyo pia imesema kuwa huenda ikatumia nguvu kumrudisha madarakani Bazoum. Ila serikali za kijeshi za Burkina Faso na Mali zilijibu kwa kusema zinaunga mkono mapinduzi ya Niger na uingiliaji wowote kutoka nje, itakuwa ni ishara ya tangazo la vita.

Vyanzo: AP/AFPE/DPAE/Reuters