1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Ufaransa kuwaondoa raia wake Niger kufuatia mapinduzi

1 Agosti 2023

Ufaransa imetangaza mpango wa kuwaondoa Niger raia wake na wa Ulaya baada ya mapinduzi ya kijeshi kufanyika nchini humo na kuungwa mkono na nchi nyingine mbili za Afrika Magharibi zinazotawaliwa na wanajeshi waasi.

https://p.dw.com/p/4UdI5
Demonstrators gather in support of the putschist soldiers in the capital Niamey
Ufaransa imeonya kuhusu mashambulizi dhidi ya raia wake NigerPicha: Balima Boureima/REUTERS

Ufaransa imetangaza mpango wa kuwaondoa nchini Niger raia wake pamoja na wa Ulaya baada ya mapinduzi ya kijeshi kufanyika kwenye taifa hilo, na kuungwa mkono na mataifa mengine mawili ya Afrika Magharibi yanayotawaliwa na wanajeshi waasi.

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imesema inawaondoa raia wake kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama Niger pamoja na ghasia zilizoelekezwa kwenye ubalozi wake mjini Niamey, baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliomuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum.

Raia kuondolewa Jumanne

Wizara hiyo imesema kufungwa kwa anga ya Niger, pia kumesababisha raia hao kushindwa kuondoka kwa kutumia njia zao wenyewe.

Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa shughuli ya kuwaondoa raia wa Ufaransa na Ulaya kwa ujumla ambao wanataka kuondoka, inaanza Jumanne na kwamba maandalizi yanaendelea. Hata hivyo, taarifa hiyo haikutoa maelezo zaidi.

Frankreich | Luis Vassy, Kabinettsdirektor des französischen Außen- und Europaministers
Maafisa wa Ufaransa wakizungumzia hali inayoendelea Niger baada ya mapinduzi ya kijeshi, kwenye mkutano uliofanyika Paris, Ufaransa Agosti 1, 2023Picha: STEFANO RELLANDINI/AFP/Getty Images

Takribani raia 600 wa Ufaransa wako Niger na wanajeshi wapatao 2,500 wa Ufaransa wanaopambana na wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu katika ukanda wa Sahel.

Siku ya Jumapili, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, aliapa kuchukua hatua za haraka iwapo raia wa Ufaransa au maslahi ya nchi hiyo yatashambuliwa, baada ya maelfu ya watu kuandamana nje ya ubalozi wa Ufaransa, mjini Niamey.

Ghasia za waandamanaji

Baadhi ya watu walijaribu kuingia ndani ya ubalozi huo, lakini walitawanywa kwa mabomu ya kutoa machozi.

Italia nayo imetangaza kuwa inatoa ndege maalum kwa ajili ya kuwaondoa raia wake Niger.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba serikali yake imechukua uamuzi huo kutokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika wiki iliyopita.

Niger | Militärputsch
Waziri wa Tawala za Mikoa na Ugatuzi wa Mali, Kanali Abdoulaye MaigaPicha: ORTM/AP/dpa/picture alliance

Hayo yanajiri wakati ambapo serikali za kijeshi za Mali na Burkina Faso zimesema uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya Niger utachukuliwa kama tangazo la vita dhidi ya mataifa hayo mawili.

Taarifa hiyo ya pamoja ilisomwa Jumatatu usiku na Waziri wa Tawala za Mikoa na Ugatuzi wa Mali, Kanali Abdoulaye Maiga, kupitia televisheni ya taifa.

Vikwazo sio halali

"Serikali za mpito za Burkina Faso na Mali, kwanza: zimeelezea mshikamano wao wa kidugu na watu wa Mali na Burkina Faso na ndugu zao wa Niger ambao wameamua kwa hiari yao wenyewe kuchukua mamlaka yao. Na pili: tunalaani mashirika ya kikanda kuweka vikwazo ambavyo vinazidisha mateso kwa wananchi," alisisitiza Kanali Maiga.

Mali na Burkina Faso zimesema vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS ni kinyume cha sheria na utu na havipaswi kutekelezwa.

(AFP, AP, DPA, Reuters)