Niger yaituhumu Ufaransa kutaka kumrejesha Bazoum madarakani
31 Julai 2023Utawala mpya wa kijeshi nchini Niger umesema Ufaransa inapanga pia kufanya mashambulizi ikulu ili kumuondoa rais Bazoum kizuizini, huku wakionya kuwa kufanya hivyo kutasababisha umwagaji mkubwa wa damu na machafuko.
Rais Mohamed Bazoum ambaye ni mshirika wa Magharibi, ameshikiliwa na jeshi tangu siku ya Jumatano wiki iliyopita.
Mkoloni wa zamani Ufaransa na Umoja wa Ulaya wamesitisha ushirikiano wa kiusalama na msaada wa kifedha kwa Niger kufuatia mapinduzi hayo, huku Marekani ikionya kuwa msaada wake pia unaweza kuwa hatarini.
Soma pia: Vikwazo vyainyemelea Niger
Umoja wa Ulaya umesema leo kuwa utawawajibisha watawala wa Niger kwa mashambulizi yote dhidi ya raia, wanadiplomasia na balozi baada ya waandamanaji wanaounga mkono mapinduzi kukusanyika na kuvamia ubalozi wa Ufaransa.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema katika taarifa yake kuwa Umoja huo utatekeleza haraka na kwa uthabiti uamuzi wa jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS na kuiwekea Niger vikwazo vya kiuchumi.
Mkutano wa ECOWAS kuhusu Niger
Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Magharibi mwa Afrika, ECOWAS wamewataka wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Niger, kurejesha utawala kwa rais Mohamed Bazoum ndani ya wiki moja.
Katika mkutano wa dharura uliofanyika jana nchini Nigeria , viongozi wa ECOWAS wamewapa wiki moja wanajeshi nchini Niger kuachia madaraka au kukabiliana na uwezekano wa matumizi ya nguvu, na kuwawekea vikwazo vya kifedha wanajeshi hao.
Soma pia: Viongozi wa ECOWAS wawaonya viongozi wa mapinduzi, Niger
Bola Tinubu, Rais wa Nigeria na mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS amesema huu si wakati wa kuendelea kutoa onyo bali ni wakati wa kuchukua hatua, huku akisisitiza kuwa Jumuiya hiyo itachukua "hatua zote" ili kurejesha utulivu wa kikatiba.
Urusi imesema hali inayoendelea Niger inatia wasiwasi mkubwa na imezitaka pande zote kujizuia na vurugu hadi kutakaporejeshwa utawala wa kisheria.
Jenerali Abdourahamane Tiani, mkuu wa kikosi cha ulinzi wa rais, amejitangaza kuwa kiongozi mpya wa Niger na kusema kuwa mapinduzi hayo ni jibu kutokana na "kuzorota kwa hali ya usalama" inayohusishwa na vitendo vya umwagaji damu vya makundi ya kigaidi, rushwa na matatizo ya kiuchumi.
Niger imeshuhudia mapinduzi ya hivi karibuni katika eneo la Sahel linalokumbwa na vitendo vya uasi wa makundi ya kigaidi na hivyo kuzusha wasiwasi mkubwa eneo hilo.