1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi za nchi za Magharibi zatoa wito kuwepo utulivu Kongo

24 Desemba 2023

Balozi za mataifa ya Magharibi zimewahimiza raia wa DR Congo kuwa watulivu baada ya viongozi wakuu wa upinzani kuutaja uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya Jumatano kama "usioaminika” huku wengine wakitaka urudiwe.

https://p.dw.com/p/4aXeR
Uchaguzi Mkuu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Denis Mukwege akipiga kura yake mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

Balozi za mataifa ya Magharibi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimewahimiza raia wa taifa hilo kuwa watulivu baada ya viongozi wakuu wa upinzani kuutaja uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya Jumatano kama "usioaminika” huku wengine wakitaka urudiwe.

Katika taarifa ya pamoja waliyoitoa jana, balozi 12 za mataifa ya magharibi katika mji mkuu Kinshasa, ikiwemo pia ubalozi wa Canada, wametoa wito wa kuwepo utulivu. 

"Madamu hivi sasa zoezi la kuhesabu kura linaendelea, tunatoa wito kwa pande zote kuwa tulivu,” balozi hizo zimeeleza.

Ubalozi wa Marekani mnamo siku ya Ijumaa pia ulitoa wito sawa na huo wa kuwepo utulivu.

Soma pia: Kongo yaanza kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi

Viongozi watano wa upinzani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametoa taarifa ya pamoja wakitaka kufanya maandamano Jumatano ijayo ili kuonyesha kutoridhishwa kwao na mchakato mzima wa uchaguzi.

Wakati huo huo, afisa mmoja wa tume ya uchaguzi CENI amesema zoezi la upigaji kura liliongezwa muda hadi siku ya Jumapili katika maeneo machache ya eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Takriban watu milioni 44 katika taifa hilo lenye idadi jumla ya watu milioni 100 wamejiandikisha kama wapiga kura, huku zaidi ya wagombea 100,000 wakijitokeza kuwania nyadhifa mbalimbali.

Rais Felix Tshisekedi mwenye umri wa miaka 60, anawania muhula mwengine madarakani dhidi ya wagombea 18 wa upinzani.

Jografia ya Kongo ni miongoni mwa changamoto katika uchaguzi

DR Kongo | Uchaguzi Mkuu Kongo 2023 | Kinshasa
Wapiga kura wakitafuta majina yao katika vituo vya kuraPicha: John Wessels/AFP/Getty Images

Ukubwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – sawa na ukubwa wa eneo zima la Ulaya Magharibi – pamoja na miundombinu mibovu kunalifanya zoezi la uchaguzi kukumbwa na changamoto kubwa ya usafirishaji wa vifaa vya kura hadi vituo vya kura.

Kuchelewa kuanza kwa upigaji kura na kuwepo kwa ukiritimba ni baadhi ya kasoro zilizozua vurugu wakati wa kuanza kwa uchaguzi mnamo siku ya Jumatano, kadhalika tume ya uchaguzi kushindwa kusafirisha vifaa vya kupigia kwa wakati na baadhi ya vituo kushindwa kufunguliwa kabisa ni baadhi tu ya changamoto zilizozikumba zoezi hilo la kidemokrasia.

Tume ya uchaguzi nchini Kongo CENI iliongeza muda wa upigaji kura hadi siku ya Alhamisi katika baadhi ya vituo ambavyo havikufunguliwa kwa wakati siku ya uchaguzi Disemba 20.

Kulingana na maafisa wa uchaguzi, upigaji kura ulikuwa unaendelea jana Jumamosi katika maeneo kadhaa, katika ishara ya kuendelea kwa matatizo yaliyolikumba zoezi zima la uchaguzi.

Soma pia: Matokeo ya uchaguzi wa rais Kongo kuanza kutangazwa

Macaire Kambau Sivikunula, afisa wa uchaguzi katika jimbo la Kivu Kaskazani mashariki mwa nchi hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, tume ya uchaguzi ya CENI ilitoa ruhusa maalum kwa vituo vitano vya kura kufunguliwa leo Jumapili kwa ajili ya kuwapa wapiga kura fursa ya kutekeleza haki yao ya kikatiba.

Kuchelewa kwa zoezi la upigaji kura kumesababisha baadhi ya maafisa wa CENI pamoja na familia zao kupokea vitisho vya kuuawa.

Viongozi watano wa upinzani wamesema katika taarifa jana kuwa, wanapanga kufanya maandamano siku ya Jumatano ijayo.

Uchaguzi DRC 2023: Matokeo ya awali yasubiriwa

Viongozi hao wa upinzani ni pamoja na daktari bingwa wa wagonjwa ya wanawake Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2018 na Martin Fayulu, mtendaji wa zamani wa kampuni ya ExxonMobil.

"Tutaandamana kuonyesha kutoridishwa kwetu na dosari zilizobainika wakati wa zoezi la upigaji kura.” Viongozi hao waliandika barua kwa gavana wa Kinshasa ambapo wanapanga kufanya maandamano.

Wagombea wengine wa upinzani akiwemo mfanyibishara na gavana wa zamani wa Kinshasa Moise Katumbi, walitoa taarifa pia wakihimiza uchaguzi huo urudiwe, wakitoa hoja kwamba umekumbwa na "udanganyifu mkubwa.”

Taifa hilo maskini la Afrika ya Kati na lenye utajiri wa madini liliandaa uchaguzi siku ya Jumatano kumchagua rais, wabunge, viongozi wa mikoa na madiwani.

Rais Felix Tshisekedi anapigiwa upatu kuchaguliwa tena hasa ikizingatiwa kuwa upinzani umegawanyika.