Ujerumani yahimiza uwajibikaji wa kimataifa ukanda wa Gaza
21 Novemba 2023Akizungumza na mwandishi wa DW Jaafar Abdul-Karim, Baerbock amehimiza jamii ya kimataifa kufanya juhudi zaidi kupunguza mzozo kwa sasa.
Aidha ametetea msimamo wa Ujerumani wa kuhimiza usitishwa wa vita kwa muda mrefu, na kusisitiza kuwa kipaumbele kwa wakati huu kinapaswa kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wakaazi wa Gaza.
Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa, pindi tu mzozo wa sasa utakapokamilika, jamii ya kimataifa inapaswa kuhakikisha hali ya utulivu inarudi katika ukanda wa Gaza ndani ya muktadha wa suluhisho la mataifa mawili kwenye mzozo wa Israel na Palestina. Ameiambia DW kuwa, "ili kuhakikisha usalama, tunahitaji uwajibikaji wa kimataifa."
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ameitembelea Israel mara tatu tangu mzozo ulipozuka mnamo Oktoba 7 wakati wanamgambo wa Hamas walipofanya shambulizi ndani ya ardhi ya Israel na kuua watu 1,200 na kuwachukua mateka watu 240.