1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tundu Lissu kurejea nchini Tanzania

14 Januari 2023

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu amesema jana kwamba atarejea nchini humo akitokea uhamishoni, nchini Ubelgiji huku akiahidi kufungua ukurasa mpya.

https://p.dw.com/p/4MBWM
Tansania Singida | Wahlen | Tundu Antiphas Lissu
Picha: Said Khamis/DW

Tundu Lissu anarejea nyumbani baada ya rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan kuondoa zuio la mikutano ya kisiasa lililowekwa na mtangulizi wake hayati John Magufuli.

Lissu amesema kwenye hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja kupitia Youtube kwamba hawana sababu ya kuendelea kuishi uhamishoni na kuongeza kuwa ana uhakika wataandika ukurasa mpya mwaka huu wa 2023 ambao ametabiri utashuhudia mabadiliko makubwa ya kihistoria nchini Tanzania.

Lissu ambaye alipigwa risasi mara 16 katika jaribio la kumuua la mwaka 2017 amekuwa akiishi nchini Ubelgiji akihofia usalama wake na ameahidi kurejea nyumbani Januari 25.

Belgien, Brüssel | Samia Suluhu Hassan, Präsidentin von Tansania in Brüssel
Tundu Lissu akiwa na rais Samia Suluhu Hassan walipokutana Brussels mwezi Februari, 2022.Picha: Sudi Mnette/Mohammed Khelef/DW

Kwa mara ya mwisho Lissu alikwenda Tanzania mwaka 2020 kwa ajili ya kugombea nafasi ya urais dhidi ya Magufuli, aliyefariki dunia miezi michache baada ya kushinda kwa awamu ya pili.

Lissu anayesifika kwa ukosoaji dhidi ya serikali ya Tanzania, alipigwa risasi mwaka 2017 akiwa kwenye gari yake mjini Dodoma nchini Tanzania.

Soma Zaidi: Mbunge wa upinzani Tanzania Lissu apigwa risasi

Rais Samia ambaye amekuwa akibadilisha baadhi ya sera tata zilizoanzishwa na mtangulizi wake, amerejesha matumaini yaliyochochea hata viongozi wa upinzani kama Lissu kurejea nyumbani. Tayari amekutana na viongozi wa upinzani ikiwa ni pamoja na Lissu mwenyewe huku Brussels mapema mwaka jana.

Lissu amenukuliwa akisema, "Rais Samia Suluhu Hassan kupitia serikali na chama chake wameonyesha utayari wa kuanzisha upya safari. Tunahitaji kuonyesha ya kwamba hata sisi tuko tayari kwa hili," alisema Lissu.

"Ninakuja nyumbani kuanza upya kwa ajili ya taifa letu."