1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lissu kurejea Tanzania kudai katiba mpya

2 Julai 2021

Licha ya Rais Samia Suluhu wa Tanzania kuweka wazi kwamba kwa wakati huu hayuko tayari kuanzisha mchakato wa katiba mpya, wapinzani wameendelea kupaza sauti kuongeza shinikizo la kudai katiba mpya.

https://p.dw.com/p/3vvWe
Tansania Wahlen | Opposition Tundu Lissu
Picha: AFP

Chama kikuu cha upinzani Tanzania, CHADEMA, kimezinduwa rasmi  Alhamis vuguvugu lake la madai ya Katiba Mpya na haki za kisiasa.

Kauli hiyo ya Rais Samia, ambaye aliwahi kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, inaonekana kama vile imeamsha ari ya wapinzani hao pamoja na wanaharakati wanaotumia majukwaa mbalimbali kupeperusha ujumbe wa kudai katiba mpya.

Chadema hakitarudi nyuma katika kutaka katiba mpya

Chadema, ambayo ilianza hivi karibuni kwa kufanya mikutano ya ndani katika takribani mikoa yote ya Tanzania Bara, sasa inaonekana kugeuza muelekeo na kuanzisha makongamano ya ndani yenye shabaha hiyo hiyo ya kushajiisha umuhimu wa kupatikana kwa katiba mpya.

Tansania Opposition Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema Freeman MbowePicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Katika kongamano lake la kwanza lenye dhima hiyo hapo jana, chama hicho kilisema hakitarudi nyuma katika mkakati wake wa kutaka kuwepo kwa katiba mpya na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, akatoa mapendekezo kadhaa kwa Rais Samia, ukiwemo ushauri wa kuunda tume ya katiba ili kusimamia mchakato wa kupata katiba mpya.

Na kwenye suala la zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, Mbowe alisema wazi kwamba hawatangojea tena, na badala yake ameitisha mikutano nchi nzima kwa ajili ya kupeleka ujumbe kudai katiba mpya.

Viongozi wa kidini nao wamekuwa wakilijadili suala la katiba mpya

Kikiweka msukumo juu ya hilo, makamu mwenyekiti wake aliyeko ugaibuni, Tundu Lissu, aliyezungumza kwa njia ya mtandao katika kongaamano hilo la kudai katiba mpya, lililofanyika kando kidogo ya kitovu cha jiji la Dar es Salaam, aliashiria utayari wake wa kurejea nchini kushiriki vuguvugu la kudai katiba mpya.

Mbali ya vyama vya siasa, pia viongozi wa kidini pamoja na watu wenye ushawishi ndani ya jamii wamekuwa wakitumia majukwaa aina mbalimbali kujadili jambo hilo, mara tu baada ya Rais Samia kuweka bayana msimamo wa serikali yake kuhusiana na madai ya katiba mpya na mikutano ya hadhara. 

CHADEMA chaomboleza kifo cha Magufuli

Ijapokuwa suala la madai ya katiba mpya limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu, lakini jambo hilo limeonekana kupata msukumo mpya katika siku za hivi karibuni na wadadisi wa mambo wanaona kwamba pengine wale wanaolipa msukumo wanajaribu kutuma ujumbe wa pekee kwa Rais Samia hasa kwa vile yeye mwenyewe amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti mwenza wa Bunge Maalumu la Katiba ambalo mchakato wake ulikwama njiani.